Yohana 14:21
"Yeye aliye na amri zangu na kuzishika yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."
Kama tukishika amri za Mungu inamaanisha tunampenda Mungu. Kumpenda Mungu ni kufuata yote aliyoyaagiza katika neno lake. Sio kuyasoma tu na kuyajua kichwani, bali kutenda kila aliloliagiza.
Kumpenda Mungu ni kwa matendo na is kwa maneno pekee. Matayo 7:16 inasema "Mtawatambua kwa matendo yao...."
Watu wengi wanaongea maneno ya Mungu lakini wapo mbali na Mungu katika matendo yao.
Kama unazishika amri za Mungu kwa vitendo inaonyesha ya kuwa mawazo yako yanafikiria zaidi kumpendeza Mungu na si kupendeza dunia na mambo yake.
Mawazo yako ni ya muhimu sana katika kukuwezesha kufanya jambo katika mwili na kuonekana. Chochote unachokifanya kimatendo , kinaanzia kwenye mawazo. Mtu hujulikana kuwa na mawazo mazuri au mabaya kutokana na matendo anayoyafanya. Ili kuweza kuwa ya mapenzi ya Mungu katika maisha yako, anza kuwaza yaliyo ya Mungu na kumtafakari Mungu na ndipo utaanza kumwamini na kufanya yale anayoyaagiza.
Mfano, Kama wewe ni mtu wa kuamka mapema asubuhi na kutafakari neno la Mungu, hii inamaana unaweka kwenye mawazo yako na akili yako ahadi na hukumu za Mungu ambazo ukizifanyia kazi utaanza kubadili mtazamo wako na baadae tabia na matendo yako yatafanana na maagizo ya Mungu.
Polepole utaanza kuachana na dhambi zilizokuwa zinakuzonga, na unaanza kuwa huru katika maeneo mbalimbali ya maisha yako.
1Yohana 2:5-6 inasema " Lakini mtu yoyote anayeshika neno la Mungu , huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana nae. Mtu yoyote anayesema ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo."
Kuna watu wanaosema wanampenda Mungu na hata wanasema wamempokea Kristo(wameokoka) lakini matendo yao yanakuwa mbali na ushuhuda wa Yesu Kristo. Lakini tukumbuke kuwa matendo ya mtu ndiyo humuelezea huyo mtu alivyo na is vinginevyo.
Nakusihi wewe mwana wa Mungu, hutakiwi kukatishwa tamaa na mtu yoyote hata kama ni mchungaji, padri, au mtumishi wa Mungu yoyote. Shetani huwa ana namna nyingi ya kutaka
kukurudisha nyuma ili usiendelee na wokovu wako. KUWA MACHO!
Kwa wewe ambaye umeamua kumkiri Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako na bado unaishi maisha ya mchanganyo, mara kwa Yesu kidogo mara duniani kidogo. ACHA!
Kwa maana Mungu amesema ukifanya hivyo atakutapika. Ufunuo 3:15 inseam " Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. afadhali ungekuwa kimojawapo: baridi au moto. Basi kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, nitakutapika!"
Ili uweze kutoka kwenye uvuguvugu huo, unatakiwa kujiuliza ni kitu gani unachoruhusu zaidi kuingia kwenye akili yako. Je ni mambo ya dunia au ni neno la Mungu.
Kama wewe ni mtu wa kupendelea kusoma magazeti ya udaku na ngono, au kuangalia picha za ngono kwenye simu au runinga au intaneti, au unapendelea kuangalia filamu za kidunia na tamthilia mbalimbali, kiukweli unakuwa ukiweka sumu ndani ya mawazo yako ya tamaa mbaya za kila namna
pamoja na hasira na chuki nk, kama inavyoonyeshwa kwenye hizo filamu.
Kumbuka mawazo yako ndiyo yanapelekea matendo yako. Tumia muda wa kutosha kujifunza mapenzi ya Mungu katika neno lake na kulitafakari, ndipo utaanza kuona polepole ukijiondoa katika mapenzi ya kidunia na kuanza kufanya mapenzi ya Mungu katika maisha yako.
Hi karibuni tuchangie ili kuweza kujifunza zaidi
ReplyDelete