"Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; wala hakusimama katika njia ya wakosaji; wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji; uzaayo matunda yake kwa majira yake; wala jani lake halinyauki. Na kila alitendalo hufanikiwa."
- Heri mtu yule kwa maana nyingine amebarikiwa mtu yule... Katika laugha ya kiebrania ni neno 'esher' ambalo lina maana mkamilifu, mwenye furaha, anayetosheka na Mungu. Heri maana yake ni furaha iliyo kuu.
Tunaweza kuona kumbe wakosaji wana mashauri, na mtu anayemjua na kumtegemea Mungu hatapokea mashauri kutoka kwa wakosaji bila kupima kama ushauri huo unaendana na makusudi ya Mungu katika neno lake.
Mashauri ya wakosaji yako mengi na yako kila mahali. Kwa mfano, kuna mashauri ya namna ya kuvaa, kulea watoto, kujilinda usipate mimba, kuishi katika ndoa, kufanya biashara gani, kujiweka utanashati na hekima nyingine nyingi za wasiomjua Mungu.
Mtu anayemjua na kumtegemea Mungu anatakiwa apate ushauri wake kutoka neno la Mungu.
2. Wala hakusimama katika njia ya wakosaji.
Wakosaji wana njia ambapo wanasimama, na mtu wa Mungu anajua hatakiwi kusimama mahali hapo. Mtu wa Mungu haogopi kutembea kwenye njia isiyopitiwa na watu wengi kwa maana anajua ndiyo njia impelekayo uzimani. Mathayo 7:13 "Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba......bali mlango ni mwembamba na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache."
Mfano wa kusimama katika njia za wakosaji ni kama ifuatavyo:
- Kushiriki maamuzi katika familia kwa mambo yasiyompendeza Mungu kama kumfanyia ubaya mmoja wa wanafamilia, kupanga njama za pamoja kuumiza wengine wanyonge katika familia nk.
- Kuchangia kwa mali vitu kwa ajili ya matambiko ya kiukoo ambayo haushiriki moja kwa moja lakini unatumia fedha zako kufanya hivyo.
- Kumpeleka mtu mwingine kwenye mambo mabaya hata kama wewe mwenyewe hushiriki
3. Kuketi barazani pa wenye mizaha
Mizaha katika maisha yetu yapo mengi sana na karibu katika kila nyanja ya maisha yetu, mizaha inaonekana. Mara nyingi mizaha inaweza ikaja au ikaonekana kama kichekesho fulani au kitu cha kufurahisha, lakini ni kitu ambacho hakimpendezi Mungu kabisa.
Mfano wa mizaha ni kama ifuatavyo:
- Kujibadilisha maumbile
- Kuongea mambo yasiyojenga kama kuna watu wanapenda kuwaita watoto wadogo "mchumba"
- Kusema uongo, uzushi, malipizi na chuki.
Mtu anayemjua Mungu hatakiwi kufanya haya. Imeandikwa katika kitabu cha 1Wathesalonike 3:13 "Apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu...."
Uneweza kushangaa kwanini haukui kiroho au kwanini maombi yako hayajibiwi, kumbe shida ni wewe upo hapo kwenye mabaraza, mizaha na njia za wakosaji.
Kama umempokea Yesu ndani ya maisha yako, wewe ni nuru. Na nuru haiwezi kuchangamana na
giza. Hii ina maana hutakiwi kushiriki mambo yoyote ya gizani. Bali unatakiwa kutafakari neno la Mungu usiku na mchana, ili uweze kujua ni nini mapenzi ya Mungu na kuweza kumzalia Mungu matunda mazuri katika maisha yako, na kufanikiwa katika kila ufanyalo.
Hi karibuni tuchangie ili kuweza kujifunza zaidi
ReplyDeleteUbarikiwe mtumishi kwa ufafanuzi wa neno hili. Amen
ReplyDeleteAsante, Karibu
ReplyDelete