Friday, 10 February 2017

Mkaribie Mungu upate haja za moyo wako

"Tazama mkono wa Bwana haukupunguka hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia. Lakini maovu yenu yamewafarakisha ninyi na Mungu wenu. Na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone; hata hataki kusikia , maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu. Midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya. Hapana adaiye kwa haki wala hapana atetaye kwa ukweli. Hutumainia ubatili, hupata mimba ya madhara na kuzaa uovu." Isaya 59:1-4

Hapa tunaona Mungu wetu ambaye ndiye Bwana wetu yuko tayari kutusikiliza na kutuokoa pale tunapopita katika taabu. Na huwa anasikia kilio chetu pale tunapomuomba. Mungu wetu si muongo , alichosema ndicho kweli na hufanyika. Yeremia 29:11-14 inasema " Maana ninayajua mawazo ninayoyawazia ninyi, asema Bwana. Ni mawazo ya amani na wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtaenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakapo nitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu asema  Bwana, nami nitawarudishia watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilipowafukuza, asema Bwana; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka."

Kinachofanya tusiuone uso wa Bwana, na kutokupata  haja za moyo wetu ni dhambi tulizonazo. Rejea Isaya 59:1-4. Dhambi tuzifanyazo kila siku kwa kuwaza, kunena na kutenda ndizo zinazotufarakanisha na Mungu wetu.
Tunajua kuwa Mungu wetu ni Mtakatifu, na hakai palipo na dhambi.
Embu chunguza mdomo wako. Ni kitu gani unachoongea kila mara? Je ni mambo ya faida au hasara, ni mambo ya kuinua au ya kuua,ni mapenzi ya Mungu au mitazamo ya duniani.
Embu chunguza mikono yako. Ni kitu gani inapendelea kushika au kufanya. Je mikono yako inatumika kwa vitu najisi au vitu vya kumpendeza Mungu. Unatumia mikono yako kuandika mambo mema au mabaya.
Embu chunguza miguu yako. Je miguu yako inakupeleka mahali gani?

Mara nyingi tunataka mguso wa Mungu, lakini maovu yetu yanauficha uso wa Bwana hata asitake kutusikia kilio chetu.
Mungu wetu yuko tayari kutusikia na kutusaidia. Tena neno linasema Mungu yupo karibu sana na sisi. Bali wewe ndiye uliyejitenga na uso wa Mungu kwa maovu unayoyafanya.

Bwana wetu Yesu Kristo alishafanya kazi yake ya kutuonyesha njia ya kwenda kwa Mungu, nayo ni kwa njia yake yeye Yesu. Kwa kumpokea Kristo Kama Bwana na mwokozi wa maisha yako ili akusamehe dhambi zako zote na uandikwe katika kitabu cha uzima cha Mungu. Na kama umeshampokea Kristo, jua ya kuwa unahitaji sasa kuishi maisha matakatifu yanayoongozwa na Roho wa Mungu.

Unachotakiwa kufanya ni kujikana kwa kuamua kuachana na chochote ambacho kinazuia uso wa Mungu kukufikia, na hizi ni dhambi za aina zozote.
Uwe ni mtu wa kujitakasa na kukaa mbali na mazoea ya kidunia ambayo yanatufanya tuwe mbali na Mungu.
Neno la Mungu linasema," Kama mkono wako ukikukosha, ung'oe....... " inamaana anza Kung'oa kila
kitu kwenye maisha yako ambayo yanakukosesha kumuona Mungu. Usipofanya hivyo utakuwa unakosa baraka kama mtoto wa Mungu.

Fanya yafuatayo: Anza kuomba rehema ya mdomo wako, miguu yako, mikono yako. Soma neno la Mungu ujue mema na mabaya. Anza kuikimbia dhambi kwa vitendo.

1 comment: