Thursday, 4 May 2017

Namna ya kumlilia Mungu katika shida yako



Zaburi 107:19-20 inasema “Wakamlilia Bwana katika shida zao. Akawaponya na shida zao.Hulituma neno lake huwaponya. Huwatoa katika maangamizi”

Ashukuriwe Mungu aliye juu kwakuwa tunalo tumaini katika yeye. Kwakuwa ndiye ngome yetu na msaada wetu wakati wa mateso.

Leo ningependa nikukumbushe kwa habari ya kumlilia Mungu katika shida uliyonayo.Kwa maana imeandikwa muite Mungu maadamu anapatikana.

Mara nyingi tunakuwa katika shida na taabu katika maisha yetu na tunakaa hapo hapo katika hiyo shida kwa muda mrefu sana kuliko ilivyotakiwa. Ni kwanini? Hii ni kwasababu hatumlilii Mungu katika shida zetu. Unaweza kujiuliza mbona huwa ninaomba sana lakini majibu hayaji. Hii pia ni kwasababu unaomba vibaya. Imeandikwa kuwa” hampati kwasababu mnaomba vibaya”.

Kuomba vibaya ni kwa namna gani?
Ni kwa kulalamika na kuliangalia tatizo lako zaidi ya kumuangalia Mungu na uweza wake wa kuliondoa tatizo. Mara nyingi unakuwa na maombi yanayotokana katika nafsi yako kuliko yanayotoka rohoni. Rohoni ni mahali pasipo na waa na ndipo Mungu hukaa. Kwenye nafsi yako ni mahali unafanya maamuzi kutokana na hali halisi inayokuzunguka. Hivyo kuomba vizuri ni kuomba sawasawa na neno la Mungu, na si mapenzi yako.
Tukiweza kuomba sawasawa na neno lake, atasikia. Mara kwa mara tunaomba sawasawa na mapenzi yetu, na ndipo Mungu hatusikiii kwasabau hujaingia bado kwenye himaya yake. Kulia sana na uchungu sana hausaidii na tena imeandikwa “uchungu wote na uondoke kwenu.”

Embu chunguza hayo unayomuomba Mungu na namna unavyomuomba, je unaomba kwa hisia ya mwilini au katika roho? Mungu ni roho, ukitaka kuongea nae uwe katika roho na ndipo Roho Mtakatifu hutusaidia pale tunaposhindwa kuomba katika roho.

Nakusihi uanze kutafuta kujua namna ya kumuomba Mungu katika roho na utaona jinsi majibu utakavyoyapata kwa haraka kama neno linavyosema walimlilia, wakaponywa na kuondolewa katika maangamizi yao.

Mungu yuko tayari kukupa hitaji lako unalomuomba, ni wewe ambaye unachelewa kujua mapenzi yake ili uweze kupata haja za moyo wako.

No comments:

Post a Comment