Kuna sababu nyingi zinazoweza kupelekea mtu kuwa na msongo wa mawazo (stress) nazo ni kama kazi, ndoa, mahusiano, familia, madeni, ugonjwa, dhambi na kutokuwajibika (procastination).
Yesu anasema kwenye neno lake "Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu." 1Petro 5:7. Soma na Zaburi 55:22.
Yesu anakutaka uishi maisha ya salama yasiyo na taabu wala shida, ndiyo maana alikuja akafa na kuchukua mizigo yetu yote pale msalabani.
Ikiwa kama utamuamini yeye na kumuachia mambo yako yote na kujikabidhi kwake, ndipo atakapochukua mizigo yako yote na kukuondolea taabu yako na kukuweka huru katika maisha yako Haleluya!
Maisha huru ni yapi? Ni yale ambayo hautawaliwi tena na dhambi. Badala yake unakuwa unatawaliwa na nguvu za Mungu na Roho Mtakatifu.
Hatua zitakazo kufanya uweze kuondoka katika msongo wa mawazo (stress) na kuishi ukiwa huru ni:-
- Muamini Yesu Kristo na awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Na utafanya hivi kwa kupitia njia tatu. Ya kwanza, kubali kuwa wewe ni mwenye dhambi. Pili, tubu dhambi zako zote kwa Yesu. Tatu, Mkaribishe Yesu aingie ndani ya maisha yako na akuongoze.
- Muamini Mungu kuwa atakutoa katika hali hiyo uliyonayo na utakuwa huru. Hapa unamwambia Mungu kila kinachokusumbua na kumkabidhi achukue hayo matatizo. Unatakiwa uwe na imani kuwa ulichomueleza Mungu amesikia na amekuondolea huo mzigo kama ni wa matatizo, taabu, shida, magonjwa, madeni nk. Angalia Zaburi 37:5, Mithali 3:5-7, Yakobo 1:6, Mathayo 21:21 na Marko 11:23
- Jitahidi kuacha dhambi. Kama kuna vitu unafanya kinyume na mapenzi ya Mungu, ACHA! Kwa maana hayo mambo ni mlango wa shetani kukutawala na kukuletea matatizo. Acha uongo, wizi, tamaa mbaya, uzinzi, kiburi, wivu, hasira, kutumia nguvu za giza nk. Angalia Wagalatia 5:19, 1Wakorintho 6:9-10.
- Soma neno la Mungu. Neno la Mungu ni taa na mwanga katika maisha yetu. Tafakari neno la Mungu. Angalia kila unachokifanya ni sawa na neno la Mungu linavyosema? Tumia angalau dakika 30 kusoma na kutafakari neno la Mungu kila siku.
- Fuata maongozo ya Roho Mtakatifu. Jifunze kusikiliza moyo wako zaidi kuliko mazingira. Kama umeshampokea Kristo, roho yako inakuwa imeungamanishwa na ya Roho Mtakatifu. Kwahiyo maamuzi mengi unayapata kwa kusikiliza nini utu wa ndani unasema na ndipo utakuwa sahihi kila wakati. Usiwe mtu wakuyumbishwa na matukio.
- Jifunze kukemea shetani, kemea mawazo mabaya, kemea maneno mabaya au mazungumzo hasi. Tumepewa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na hawatatudhuru. Luka10:9, Mithali 21:23
- Tafuta mtumishi wa Mungu unayemuamini atakayeweza kukufundisha mambo muhimu ya kuzingatia usije ukarudi nyuma. Mtumishi wa Mungu ni mtu yoyote unayemuona amekuzidi kiroho na maisha yake yana ushuhuda wa Yesu Kristo na ungependa na wewe akufanye kama yeye katika kumtafuta Mungu. Siyo lazima awe mchungaji.
Mpendwa, kuishi maisha ya uhuru ndani ya Kristo ni uchaguzi au maamuzi ambayo unatakiwa kufanya kwa hiari yako. Kuna wengi wamempokea Yesu lakini hawajaamua kuishi kwa uhuru mbali na matatizo kwasababu hawajaachana na mambo yanayoendelea kuwapa shida. Nakushauri utumie kanuni hizi chache na utaanza kuona vifungo mbalimbali vikikuachia na pole pole utaanza kuishi maisha ya ushindi bila msongo wa mawazo.
Hi karibuni tuchangie ili kuweza kujifunza zaidi
ReplyDelete