Monday, 13 February 2017

Kuwa kiumbe kipya

2Wakorintho 5:17
"Hata imekuwa mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya."

Yesu Kristo alikwenda msalabani kwa ajili ya kuchukua maovu yetu, madhaifu yetu, magonjwa yetu, maumivu yetu na kushindwa kwetu. Yesu alipochukua haya yote kutoka kwetu, alituachia uhuru mbali na yote yaliyokuwa yanatusumbua.
Kwahiyo kama umempokea huyu Yesu ujue yakuwa umepokea package yako ya uhuru mbali na yote yaliyokuwa yanakusumbua wakati ukiwa gizani. Iwe ni magonjwa, laana, umasikini, kushindwa, huzuni, woga nk.
Jua kabisa Bwana Yesu alishamaliza kazi yake pale msalabani ya kukufanya uwe huru na mshindi dhidi ya dhambi na mambo mengine mengi katika maisha yako. Unachotakiwa kufanya ni kuamini kazi aliyoifanya pale msalabani, na kuipokea kwa Imani kuwa ni ya kwako na itakuwa yako.

Kazi kubwa ambayo Yesu ametuachia ni kupumzika katika kazi aliyoifanya pale msalabani. Waebrania 4:9-11 " Basi imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu......Basi na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yoyote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi."

Sabato wetu ni Yesu Kristo. Na tunaambiwa tufanye bidii kuingia na kuamini huyo sabato ambaye ni Yesu pamoja na kazi aliyoifanya pale msalabani ili kuweza kupata tunachohitaji.

Watu wengi waliompokea Kristo wameishia tu pale msalabani ambapo dhambi zao zimechukuliwa. Nakweli wamesamehewa dhambi na wako huru kwa habari ya hatia walizokuwa nazo. Lakini sasa tunatakiwa tuendelee mbele katika Kristo mfufuka ambaye kwasasa ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba. Akiwa mwenye nguvu na mshindi dhidi ya shetani.

Nakusihi mwana wa Mungu, Anza kujiona kuwa na wewe ni mshindi katika maisha yako. Anza kuona na kuipokea ile kazi ambayo unaitamani. Anza kuona ukifanya mambo makubwa katika maisha yako. Anza kuona uponyaji wa mwili wako na namna utakavyokuwa huru mbali na hayo magonjwa.

Hili neno la Waebrania linasema tufanye bidii kuingia kwenye hiyo raha. Napenda namna New King James bible alivyoiweka v10 " For he who has entered His rest has himself also ceased from his works as God did from His"
Tunatakiwa tusijitahidi kwa nguvu zetu kufanya mambo yaende, bali tunatakiwa kupokea kwa shukrani ile kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani na kwa imani tutakuwa huru.

Je unaumwa popote katika mwili wako, bidii yako iwe ni kupokea uponyaji wako kutoka msalabani kwa maana maandiko yanasema kwa kupigwa kwake tulipona. Jua ya kuwa ulikushapona miaka 2017 iliyopita. Pokea uponyaji wako na uukiri uponyaji na kuufurahia.

Je una mzigo wa uchungu na kukataliwa na watu. Usilie tena. Yesu alishachukua mizigo yako yote pale msalabani. Pokea amani yake ndani ya moyo wako sasa kwa jina la Yesu. Amini kazi aliyoifanya na uitafakari hiyo tu na uhuru wako utauona.

Unachotakiwa kufanya ili kuona matokeo ya kuwa kiumbe kipya, ni kuamini kazi aliyoifanya Yesu pale msalabani na kuitafakari usiku na mchana ili ufanane nayo. Achana na kutafakari mambo yanayo kuumiza. Anza kutafakari ukuu wa Mungu na Ahadi zake katika maisha yako na polole utaona unavyopokea kile kitu unachomuomba Mungu akupatie kama ni uponyaji, kazi, mke, mme, watoto, biashara, tabia nzuri nk. Waefeso 3: 20 inasema "Basi atukuzwe Yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu."


1 comment: