Monday, 27 February 2017

Jehanamu ya moto ni halisi

Tusome Mathayo 5:21-22
Msatari wa 22 unasema jehanamu ya moto. Haya ni maneno aliyoyasema Yesu Kristo mwenyewe yakuwa jehanamu ya moto ipo. Hatakama huamini, haitabadilisha.

Kwanini jehanamu ya moto?
Hii ni sehemu ambayo Mungu ameiandaa kwa ajili ya shetani na malaika zake. Ni sehemu ambayo ilikusudiwa kwa ajili ya watenda maovu ambao wako kinyume na Mungu mwenyenzi. Na ndiyo maana pia kuna wanadamu ambao nao wataenda huko wale ambao hawamwabudu Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo.

Je unajitayarishaje kwa ajili ya ulimwengu ujao?
Najua unajitayarisha kwa habari ya maisha yako ya hapa duniani kama kujenga nyumba kwa ajili ya familia, kupata elimu mbalimbali, kuishi vizuri na watu nk. Lakini je unajitayarisha pia kwa habari ya maisha yako ya baada ya kifo? Je unajua ukifa utaenda wapi?
Ni watu wengi sana wanaokufa kila dakika. Walio wengi hawajui ni wapi wanakwenda, wanajikuta tayari wapo kwenye maisha mengine. Je ni wangapi unaowajua walikufa wakiwa dhambini? Hawajampa Yesu Kristo maisha  yao? Hivi unafikiri mtu huyo ataenda wapi bila Yesu?

Tuangalie Luka 16 kwa habari ya yule tajiri na Lazaro. Yule tajiri alipokufa, alijikuta yuko Jehanamu ya moto. Na akatamani kurudi duniani kuwaambia watu wa nyumbani kwake kuwa wasiende huko aliko. Hapa tunaona tajiri huyu ni kama anatuambia tujitayarishe hapa duniani tusisubiri kujionea  hukohuko tukifika baada ya maisha haya.

Mpendwa jiandae! Tumeambiwa katika maandiko matakatifu yakuwa baada ya kifo ni hukumu. Yaani hukumu ya jehanamu ya moto au raha ya mbinguni katika Kristo Yesu.
Tunapaswa kujiandaa hapahapa duniani. Safari yako ya umilele ilishaanza toka pale ulipozaliwa. Wewe ni roho, na hapa duniani unaishi ndani ya mwili. Mwili huu ukifa utazikwa lakini wewe ambaye ni roho utaendelea kuishi na kupewa mwili mpya kutokana na sehemu utakayoelekea.
Uchaguzi ni wako mpendwa wangu. Embu kaa na utafakari mahali dunia na fahari yake yote itakapokupeleka. Mchague Yesu leo awe ndiyo kimbilio lako na maisha yako. Mwache Yesu ayatawale maisha yako sasa ili uweze kuongozwa nae kuishi vizuri hapa duniani na baadae kwenye uzima wa milele ujao.

Jua kwamba njia ya kwenda jehanamu ya moto ni pana na ni rahisi sana kuiendea. Njia ya mbinguni kwa Mungu ni nyembamba na wanaoiendea njia hii kamwe hawawezi kufanana na wale wa njia pana. Kwasababu hekima za hizi sehemu mbili ni tofauti. Njia pana inaongozwa na shetani wakati njia nyembamba inaongozwa na Roho Mtakatifu.

Haijalishi kuwa wewe ni mtumishi wa Mungu kama padri, mchungaji au mwamini. Kama hujajiweka tayari na kuiendea njia nyembamba, utajikuta uko njia pana tu itakayokupeleka jehanamu ya moto. Kuwa macho! 

Jehanamu ya moto ipo. Nakusihi usiende huko. Hauhitaji kwenda huko. Mpokee Yesu leo upate kubadilisha maisha yako na kumuishia yeye.

Wednesday, 15 February 2017

Je wewe ni mmoja wa Kanisa litakalonyakuliwa na Yesu

Hii ina maana gani?

Kitambo kidogo kinakuja ambapo kanisa la Mungu, wale waliompokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao na kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu katika kila eneo la maisha yao, watanyakuliwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu kuelekea mawinguni kumlaki Bwana Yesu, pale panda itakapolia. Nao wataelekea mbinguni kwenye karamu ya Mwanakondoo, na Kanisa ndilo Bibi harusi. (1Wathesalonike 4:17, Matendo ya mitume1:11)

Kitu gani cha kufanya ili kuwa mmoja wa Kanisa la Bwana Yesu Kristo?

Mpokee Yesu Kristo ndani ya maisha yako na yeye awe Bwana na Mwokozi wako hivyo ulivyo. Yesu Kristo atakupokea na kukusafishana damu yake na kukuwezesha kuishi maisha ya mabadiliko ya kumpendeza yeye. (Warumi 3:23, Warumi 6:23, Warumi 5:8, Warumi 10:13, Warumi 10:11,Mathayo 10:32)

Kitu gani hutokea ukimpokea Kristo ndani ya moyo wako?

  • Unapata msamaha wa dhambi zako zote, jina lako linaandikwa katika kitabu cha Mungu.
  • Utampokea Roho Mtakatifu atakayekufundisha njia ya kumpendeza Mungu  na kukupa ushindi juu ya dhambi, tamaa za dunia na shetani.
  • Utaishi kwa matumaini bila woga
  • Utapata furaha ya ndani ya moyo na amani hata kama unapitia magumu
  • Utaanza kujua siri za Mungu kuhusu majira na nyakati muhimu zinazohusu watu wake yaani Kanisa na Israel.
  • Unakuwa katika hali yakuwa tayari kukutana naYesu ajapo kuchukua walio wake hapa duniani.
Kitu gani hutokea usipo mpokea Yesu Kristo ndani ya moyo wako?
  • Unaishi maisha ya woga na kukosa matumaini ya siku zijazo
  • Unaishi kwa kutegemea uweza wako na wa wengine
  • Unakuwa bize na mafanikio ya duniani
  • Hupendelei kusikiliza neno la Mungu
  • Unakuwa hauna taarifa ya namna ya kujitayarisha kwa ujio wa Bwana Yesu
  • Utaachwa duniani wakati kanisa linachukuliwa na Bwana Yesu kuelekea mbinguni
Kama utapenda kumpokea BwanaYesu ndani ya moyo wako, sali sala hii kwa kumaanisha.

Bwana Yesu, nakuja mbele zako kwa moyo wangu wote na kwa akili zangu zote. Naomba unisamehe dhambi zangu zote. Asante kwa kufa msalabani kwa ajili yangu. Nakupokea sasa ndani ya moyo wangu na maisha yangu. Damu yako ya thamani na initakase iniweke huru sasa mbali na dhambi. Niponye na magonjwa yote. Futa jina langu katika kitabu cha hukumu. Andika jina langu katika kitabu cha uzima cha mwanakondoo. Nijaze na Roho Mtakatifu anifundishe kukujua wewe. Naomba haya kwa jina la Yesu Kristo. Amen.

Kama umeomba sala hii kwa kumaanisha, umempokea Bwana Yesu ndani ya moyo wako. Umekuwa mmoja wa kanisa la Mungu hapa duniani. Omba uongozi wa Roho Mtakatifu kila siku. Pia unaweza kunijulisha kwa kunitumia barua pepe integritythewaytosuccess@gmail.com au nipigie kwenye 
255 782 880 330/ 255 758 764 539

Ondoa Msongo wa Mawazo kibiblia

Msongo wa mawazo yaani stress hutokea pale ambapo mwili unapotoa homoni za kuweza kupigana na hiyo hali ya msongo wa mawazo. Hiyo hali ikiwa inaendelea sana ndiyo mtu anapatwa na msongo wa mawazo, ambapo mwili wake unakuwa hauna nguvu ya kupigana tena na unakuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa.

Kuna sababu nyingi zinazoweza kupelekea mtu kuwa na msongo wa mawazo (stress) nazo ni kama kazi, ndoa, mahusiano, familia, madeni, ugonjwa, dhambi na kutokuwajibika (procastination).

Yesu anasema kwenye neno lake "Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu." 1Petro 5:7. Soma na Zaburi 55:22.
Yesu anakutaka uishi maisha ya salama yasiyo na taabu wala shida, ndiyo maana alikuja akafa na kuchukua mizigo yetu yote pale msalabani.
Ikiwa kama utamuamini yeye na kumuachia mambo yako yote na kujikabidhi kwake, ndipo atakapochukua mizigo yako yote na kukuondolea taabu yako na kukuweka huru katika maisha yako Haleluya!

Maisha huru ni yapi? Ni yale ambayo hautawaliwi tena na dhambi. Badala yake unakuwa unatawaliwa na nguvu za Mungu na Roho Mtakatifu.

Hatua zitakazo kufanya uweze kuondoka katika msongo wa mawazo (stress) na kuishi ukiwa huru ni:-

  • Muamini Yesu Kristo na awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Na utafanya hivi kwa kupitia njia tatu. Ya kwanza, kubali kuwa wewe ni mwenye dhambi. Pili, tubu dhambi zako zote kwa Yesu. Tatu, Mkaribishe Yesu aingie ndani ya maisha yako na akuongoze.
  • Muamini Mungu kuwa atakutoa katika hali hiyo uliyonayo na utakuwa huru. Hapa unamwambia Mungu kila kinachokusumbua na kumkabidhi achukue hayo matatizo. Unatakiwa uwe na imani kuwa ulichomueleza Mungu amesikia na amekuondolea huo mzigo kama ni wa matatizo, taabu, shida, magonjwa, madeni nk. Angalia Zaburi 37:5, Mithali 3:5-7, Yakobo 1:6, Mathayo 21:21 na Marko 11:23
  • Jitahidi kuacha dhambi. Kama kuna vitu unafanya kinyume na mapenzi ya Mungu, ACHA! Kwa maana hayo mambo ni mlango wa shetani kukutawala na kukuletea matatizo. Acha uongo, wizi, tamaa mbaya, uzinzi, kiburi, wivu, hasira, kutumia nguvu za giza nk. Angalia Wagalatia 5:19, 1Wakorintho 6:9-10.
  • Soma neno la Mungu. Neno la Mungu ni taa na mwanga katika maisha yetu. Tafakari neno la Mungu. Angalia kila unachokifanya ni sawa na neno la Mungu linavyosema? Tumia angalau dakika 30 kusoma na kutafakari neno la Mungu kila siku.
  • Fuata maongozo ya Roho Mtakatifu. Jifunze kusikiliza moyo wako zaidi kuliko mazingira. Kama umeshampokea Kristo, roho yako inakuwa imeungamanishwa na ya Roho Mtakatifu. Kwahiyo maamuzi mengi unayapata kwa kusikiliza nini utu wa ndani unasema na ndipo utakuwa sahihi kila wakati. Usiwe mtu wakuyumbishwa na matukio.
  • Jifunze kukemea shetani, kemea mawazo mabaya, kemea maneno mabaya au mazungumzo hasi. Tumepewa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na hawatatudhuru. Luka10:9, Mithali 21:23
  • Tafuta mtumishi wa Mungu unayemuamini atakayeweza kukufundisha mambo muhimu ya kuzingatia usije ukarudi nyuma. Mtumishi wa Mungu ni mtu yoyote unayemuona amekuzidi kiroho na maisha yake yana ushuhuda wa Yesu Kristo na ungependa na wewe akufanye kama yeye katika kumtafuta Mungu. Siyo lazima awe mchungaji. 
Mpendwa, kuishi maisha ya uhuru ndani ya Kristo ni uchaguzi au maamuzi ambayo unatakiwa kufanya kwa hiari yako. Kuna wengi wamempokea Yesu lakini hawajaamua kuishi kwa uhuru mbali na matatizo kwasababu hawajaachana na mambo yanayoendelea kuwapa shida. Nakushauri utumie kanuni hizi chache na utaanza kuona vifungo mbalimbali vikikuachia na pole pole utaanza kuishi maisha ya ushindi bila msongo wa mawazo.

Monday, 13 February 2017

Kuwa kiumbe kipya

2Wakorintho 5:17
"Hata imekuwa mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya."

Yesu Kristo alikwenda msalabani kwa ajili ya kuchukua maovu yetu, madhaifu yetu, magonjwa yetu, maumivu yetu na kushindwa kwetu. Yesu alipochukua haya yote kutoka kwetu, alituachia uhuru mbali na yote yaliyokuwa yanatusumbua.
Kwahiyo kama umempokea huyu Yesu ujue yakuwa umepokea package yako ya uhuru mbali na yote yaliyokuwa yanakusumbua wakati ukiwa gizani. Iwe ni magonjwa, laana, umasikini, kushindwa, huzuni, woga nk.
Jua kabisa Bwana Yesu alishamaliza kazi yake pale msalabani ya kukufanya uwe huru na mshindi dhidi ya dhambi na mambo mengine mengi katika maisha yako. Unachotakiwa kufanya ni kuamini kazi aliyoifanya pale msalabani, na kuipokea kwa Imani kuwa ni ya kwako na itakuwa yako.

Kazi kubwa ambayo Yesu ametuachia ni kupumzika katika kazi aliyoifanya pale msalabani. Waebrania 4:9-11 " Basi imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu......Basi na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yoyote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi."

Sabato wetu ni Yesu Kristo. Na tunaambiwa tufanye bidii kuingia na kuamini huyo sabato ambaye ni Yesu pamoja na kazi aliyoifanya pale msalabani ili kuweza kupata tunachohitaji.

Watu wengi waliompokea Kristo wameishia tu pale msalabani ambapo dhambi zao zimechukuliwa. Nakweli wamesamehewa dhambi na wako huru kwa habari ya hatia walizokuwa nazo. Lakini sasa tunatakiwa tuendelee mbele katika Kristo mfufuka ambaye kwasasa ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba. Akiwa mwenye nguvu na mshindi dhidi ya shetani.

Nakusihi mwana wa Mungu, Anza kujiona kuwa na wewe ni mshindi katika maisha yako. Anza kuona na kuipokea ile kazi ambayo unaitamani. Anza kuona ukifanya mambo makubwa katika maisha yako. Anza kuona uponyaji wa mwili wako na namna utakavyokuwa huru mbali na hayo magonjwa.

Hili neno la Waebrania linasema tufanye bidii kuingia kwenye hiyo raha. Napenda namna New King James bible alivyoiweka v10 " For he who has entered His rest has himself also ceased from his works as God did from His"
Tunatakiwa tusijitahidi kwa nguvu zetu kufanya mambo yaende, bali tunatakiwa kupokea kwa shukrani ile kazi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani na kwa imani tutakuwa huru.

Je unaumwa popote katika mwili wako, bidii yako iwe ni kupokea uponyaji wako kutoka msalabani kwa maana maandiko yanasema kwa kupigwa kwake tulipona. Jua ya kuwa ulikushapona miaka 2017 iliyopita. Pokea uponyaji wako na uukiri uponyaji na kuufurahia.

Je una mzigo wa uchungu na kukataliwa na watu. Usilie tena. Yesu alishachukua mizigo yako yote pale msalabani. Pokea amani yake ndani ya moyo wako sasa kwa jina la Yesu. Amini kazi aliyoifanya na uitafakari hiyo tu na uhuru wako utauona.

Unachotakiwa kufanya ili kuona matokeo ya kuwa kiumbe kipya, ni kuamini kazi aliyoifanya Yesu pale msalabani na kuitafakari usiku na mchana ili ufanane nayo. Achana na kutafakari mambo yanayo kuumiza. Anza kutafakari ukuu wa Mungu na Ahadi zake katika maisha yako na polole utaona unavyopokea kile kitu unachomuomba Mungu akupatie kama ni uponyaji, kazi, mke, mme, watoto, biashara, tabia nzuri nk. Waefeso 3: 20 inasema "Basi atukuzwe Yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu."


Sunday, 12 February 2017

Ana heri mtu huyu

Zaburi1: 1-3
"Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; wala hakusimama katika njia ya wakosaji; wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji; uzaayo matunda yake kwa majira yake; wala jani lake halinyauki. Na kila alitendalo hufanikiwa."


  1. Heri mtu yule kwa maana nyingine amebarikiwa mtu yule... Katika laugha ya kiebrania ni neno 'esher' ambalo lina maana mkamilifu, mwenye furaha, anayetosheka na Mungu. Heri maana yake ni furaha iliyo kuu.


Tunaweza kuona kumbe wakosaji wana mashauri, na mtu anayemjua na kumtegemea Mungu hatapokea mashauri kutoka kwa wakosaji bila kupima kama ushauri huo unaendana na makusudi ya Mungu katika neno lake.
Mashauri ya wakosaji yako mengi na yako kila mahali. Kwa mfano, kuna mashauri ya namna ya kuvaa, kulea watoto, kujilinda usipate mimba, kuishi katika ndoa, kufanya biashara gani, kujiweka utanashati na hekima nyingine nyingi za wasiomjua Mungu.
Mtu anayemjua na kumtegemea Mungu anatakiwa apate ushauri wake kutoka neno la Mungu.

     2.   Wala hakusimama katika njia ya wakosaji.

Wakosaji wana njia ambapo wanasimama, na mtu wa Mungu anajua hatakiwi kusimama mahali hapo. Mtu wa Mungu haogopi kutembea kwenye njia isiyopitiwa na watu wengi kwa maana anajua ndiyo njia impelekayo uzimani. Mathayo 7:13 "Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba......bali mlango ni mwembamba na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache."
Mfano wa kusimama katika njia za wakosaji ni kama ifuatavyo:

  • Kushiriki maamuzi katika familia kwa mambo yasiyompendeza Mungu kama kumfanyia ubaya mmoja wa wanafamilia, kupanga njama za pamoja kuumiza wengine wanyonge katika familia nk.
  • Kuchangia kwa mali vitu kwa ajili ya matambiko ya kiukoo ambayo haushiriki moja kwa moja lakini unatumia fedha zako kufanya hivyo.
  • Kumpeleka mtu mwingine kwenye mambo mabaya hata kama wewe mwenyewe hushiriki
       3.   Kuketi barazani pa wenye mizaha
Mizaha katika maisha yetu yapo mengi sana na karibu katika kila nyanja ya maisha yetu, mizaha inaonekana. Mara nyingi mizaha inaweza ikaja au ikaonekana kama kichekesho fulani au kitu cha kufurahisha, lakini ni kitu ambacho hakimpendezi Mungu kabisa.
Mfano wa mizaha ni kama ifuatavyo:
  • Kujibadilisha maumbile
  • Kuongea mambo yasiyojenga kama kuna watu wanapenda kuwaita watoto wadogo "mchumba"
  • Kusema uongo, uzushi, malipizi na chuki.
Mtu anayemjua Mungu hatakiwi kufanya haya. Imeandikwa katika kitabu cha 1Wathesalonike 3:13 "Apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu...."

Uneweza kushangaa kwanini haukui kiroho au kwanini maombi yako hayajibiwi, kumbe shida ni wewe upo hapo kwenye mabaraza, mizaha na njia za wakosaji.

Kama umempokea Yesu ndani ya maisha yako, wewe ni nuru. Na nuru haiwezi kuchangamana na 
giza. Hii ina maana hutakiwi kushiriki mambo yoyote ya gizani. Bali unatakiwa kutafakari neno la Mungu usiku na mchana, ili uweze kujua ni nini mapenzi ya Mungu na kuweza kumzalia Mungu matunda mazuri katika maisha yako, na kufanikiwa katika kila ufanyalo.





Friday, 10 February 2017

Tenda Neno la Mungu Kuwa HURU!


Yohana 14:21
"Yeye aliye na amri zangu na kuzishika yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."

Kama tukishika amri za Mungu inamaanisha tunampenda Mungu. Kumpenda Mungu ni kufuata yote aliyoyaagiza katika neno lake. Sio kuyasoma tu na kuyajua kichwani, bali kutenda kila aliloliagiza.
Kumpenda Mungu ni kwa matendo na is kwa maneno pekee. Matayo 7:16 inasema "Mtawatambua kwa matendo yao...."
Watu wengi wanaongea maneno ya Mungu lakini wapo mbali na Mungu katika matendo yao.
Kama unazishika amri za Mungu kwa vitendo inaonyesha ya kuwa mawazo yako yanafikiria zaidi kumpendeza Mungu na si kupendeza dunia na mambo yake.
Mawazo yako ni ya muhimu sana katika kukuwezesha kufanya jambo katika mwili na kuonekana. Chochote unachokifanya kimatendo , kinaanzia kwenye mawazo. Mtu hujulikana kuwa na mawazo mazuri au mabaya kutokana na matendo anayoyafanya. Ili kuweza kuwa ya mapenzi ya Mungu katika maisha yako, anza kuwaza yaliyo ya Mungu na kumtafakari Mungu na ndipo utaanza kumwamini na kufanya yale anayoyaagiza.
Mfano, Kama wewe ni mtu wa kuamka mapema asubuhi na kutafakari neno la Mungu, hii inamaana unaweka kwenye mawazo yako na akili yako ahadi na hukumu za Mungu ambazo ukizifanyia kazi utaanza kubadili mtazamo wako na baadae tabia na matendo yako yatafanana na maagizo ya Mungu.
Polepole utaanza kuachana na dhambi zilizokuwa zinakuzonga, na unaanza kuwa huru katika maeneo mbalimbali ya maisha yako.

1Yohana 2:5-6 inasema " Lakini mtu yoyote anayeshika neno la Mungu , huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana nae. Mtu yoyote anayesema ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo."

Kuna watu wanaosema wanampenda Mungu na hata wanasema wamempokea Kristo(wameokoka) lakini matendo yao yanakuwa mbali na ushuhuda wa Yesu Kristo. Lakini tukumbuke kuwa matendo ya mtu ndiyo humuelezea huyo mtu alivyo na is vinginevyo.

Nakusihi wewe mwana wa Mungu, hutakiwi kukatishwa tamaa na mtu yoyote hata kama ni mchungaji, padri, au mtumishi wa Mungu yoyote. Shetani huwa ana namna nyingi ya kutaka
kukurudisha nyuma ili usiendelee na wokovu wako. KUWA MACHO!

Kwa wewe ambaye umeamua kumkiri Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako na bado unaishi maisha ya mchanganyo, mara kwa Yesu kidogo mara duniani kidogo. ACHA!
Kwa maana Mungu amesema ukifanya hivyo atakutapika. Ufunuo 3:15 inseam " Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. afadhali ungekuwa kimojawapo: baridi au moto. Basi kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, nitakutapika!"

Ili uweze kutoka kwenye uvuguvugu huo, unatakiwa kujiuliza ni kitu gani unachoruhusu zaidi kuingia kwenye akili yako. Je ni mambo ya dunia au ni neno la Mungu.
Kama wewe ni mtu wa kupendelea kusoma magazeti ya udaku na ngono, au kuangalia picha za ngono kwenye simu au runinga au intaneti, au unapendelea kuangalia filamu za kidunia na tamthilia mbalimbali, kiukweli unakuwa ukiweka sumu ndani ya mawazo yako ya tamaa mbaya za kila namna
pamoja na hasira na chuki nk, kama inavyoonyeshwa kwenye hizo filamu.

Kumbuka mawazo yako ndiyo yanapelekea matendo yako. Tumia muda wa kutosha  kujifunza mapenzi ya Mungu katika neno lake na kulitafakari, ndipo utaanza kuona polepole ukijiondoa katika mapenzi ya kidunia na kuanza kufanya  mapenzi ya Mungu katika maisha yako. 


Mkaribie Mungu upate haja za moyo wako

"Tazama mkono wa Bwana haukupunguka hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia. Lakini maovu yenu yamewafarakisha ninyi na Mungu wenu. Na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone; hata hataki kusikia , maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu. Midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya. Hapana adaiye kwa haki wala hapana atetaye kwa ukweli. Hutumainia ubatili, hupata mimba ya madhara na kuzaa uovu." Isaya 59:1-4

Hapa tunaona Mungu wetu ambaye ndiye Bwana wetu yuko tayari kutusikiliza na kutuokoa pale tunapopita katika taabu. Na huwa anasikia kilio chetu pale tunapomuomba. Mungu wetu si muongo , alichosema ndicho kweli na hufanyika. Yeremia 29:11-14 inasema " Maana ninayajua mawazo ninayoyawazia ninyi, asema Bwana. Ni mawazo ya amani na wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtaenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakapo nitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu asema  Bwana, nami nitawarudishia watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilipowafukuza, asema Bwana; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka."

Kinachofanya tusiuone uso wa Bwana, na kutokupata  haja za moyo wetu ni dhambi tulizonazo. Rejea Isaya 59:1-4. Dhambi tuzifanyazo kila siku kwa kuwaza, kunena na kutenda ndizo zinazotufarakanisha na Mungu wetu.
Tunajua kuwa Mungu wetu ni Mtakatifu, na hakai palipo na dhambi.
Embu chunguza mdomo wako. Ni kitu gani unachoongea kila mara? Je ni mambo ya faida au hasara, ni mambo ya kuinua au ya kuua,ni mapenzi ya Mungu au mitazamo ya duniani.
Embu chunguza mikono yako. Ni kitu gani inapendelea kushika au kufanya. Je mikono yako inatumika kwa vitu najisi au vitu vya kumpendeza Mungu. Unatumia mikono yako kuandika mambo mema au mabaya.
Embu chunguza miguu yako. Je miguu yako inakupeleka mahali gani?

Mara nyingi tunataka mguso wa Mungu, lakini maovu yetu yanauficha uso wa Bwana hata asitake kutusikia kilio chetu.
Mungu wetu yuko tayari kutusikia na kutusaidia. Tena neno linasema Mungu yupo karibu sana na sisi. Bali wewe ndiye uliyejitenga na uso wa Mungu kwa maovu unayoyafanya.

Bwana wetu Yesu Kristo alishafanya kazi yake ya kutuonyesha njia ya kwenda kwa Mungu, nayo ni kwa njia yake yeye Yesu. Kwa kumpokea Kristo Kama Bwana na mwokozi wa maisha yako ili akusamehe dhambi zako zote na uandikwe katika kitabu cha uzima cha Mungu. Na kama umeshampokea Kristo, jua ya kuwa unahitaji sasa kuishi maisha matakatifu yanayoongozwa na Roho wa Mungu.

Unachotakiwa kufanya ni kujikana kwa kuamua kuachana na chochote ambacho kinazuia uso wa Mungu kukufikia, na hizi ni dhambi za aina zozote.
Uwe ni mtu wa kujitakasa na kukaa mbali na mazoea ya kidunia ambayo yanatufanya tuwe mbali na Mungu.
Neno la Mungu linasema," Kama mkono wako ukikukosha, ung'oe....... " inamaana anza Kung'oa kila
kitu kwenye maisha yako ambayo yanakukosesha kumuona Mungu. Usipofanya hivyo utakuwa unakosa baraka kama mtoto wa Mungu.

Fanya yafuatayo: Anza kuomba rehema ya mdomo wako, miguu yako, mikono yako. Soma neno la Mungu ujue mema na mabaya. Anza kuikimbia dhambi kwa vitendo.