Wednesday, 24 May 2017

Kumwabudu Mungu katika roho na kweli



Yohana 4:23
“Lakini saa inakuja, nayo saa ipo ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katila roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”

Katika mstari huu tunaweza kuona ya kuwa kuna waabudio halisi. Na kama kuna waabudio halisi pia kutakuwa na waabudio wasio halisi. Pia inasema waabudio halisi ni wachache na ndiyo maana Baba anawatafuta hao ili wamwabudu.

Je ni kwa namna gani unaweza kumwabudu Mungu?

Ni kwa kuishi maisha ya rohoni katika kila nyanja ya maisha yako. Iwe kwa kusema kwako, kwa kutenda kwako na kutembea kwako.
Kuabudu anakokutaka Mungu Baba ni kule kunakotoka katika roho yako na siyo katika nafsi yako. Tofauti ni kuwa, kwenye nafsi yako ndiko kunakotoka kufikiri kwako na kuona mantiki ya kitu kutokana na mazingira yanayokuzunguka, watu wanavyosema au wewe unavyojisikia.

Kwenye roho yako ni mahali ambapo ni pa ukweli unaotokana na neno la Mungu, roho huangalia neno na si mazingira. Ndiyo maana hata ukiwa katika taabu unatakiwa ufurahie kwasababu neno linasema hivyo. Kwenye roho hakuna kikomo ni utimilifu tu na ukiamini na kuishi katika roho, hakika utakuwa ni mtu wa kuishi maisha ya ushindi tu kila siku.

Utajuaje kama unamuabudu Mungu katika roho na kweli au la.

Mtu asiyemwabudu Mungu katika roho anakuwa anaabudu kutokana na mazingira yanayomzunguka. Mfano umefaulu shule ndipo unamuabudu kwasababu hiyo, au unauchungu fulani ndipo unaingia kumuabudu Mungu kutokana na hisia ulizonazo na kulia kwa uchungu.



Mara nyingi hata nyimbo za kuabudu unakuta zinaimbwa lakini maneno yake unakuta yanatuongelea sisi na maisha yetu badala ya kumuongelea Mungu na uweza wake. Kwahiyo unakuta mtu anavuta hisia ya vitu vinavyomzunguka na kupata msisimko akifikiri anamuabudu Mungu kumbe la hasha.

Kumuabudu Mungu katika roho na kweli siyo tukio (event), bali ni maisha ya kila siku na kila wakati. Hii ina maana unamwabudu Mungu kwa jinsi alivyo yeye pekee, uweza wake, ukuu wake, bila kuruhusu akili yako kusikiliza hisia zinazokuzunguka.


Tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kumwabudu Mungu katika roho na kweli ambapo tutamuangalia yeye tu na uweza wake pasipo kuangalia magumu yaliyotuzunguka.

2 comments:

  1. Karibu utoe maoni yako kuhusu kumwabudu Mungu

    ReplyDelete
  2. Glory to God Mungu atuwezeshe katika hili la kumwabudu yeye katika roho na kweli hakika ni somo nzuri

    ReplyDelete