Habari msomaji wangu,
Karibu kwenye somo la leo.
Tunasoma kutoka kitabu cha Yeremia 34 kinachoongelea jinsi
Mungu mwenyenzi alipoongea na nabii Yeremia na kumpa maagizo yake ili awaambie
watu wa Yuda wakaao Israeli nini Mungu anapenda wafanye.
Lakini ukiendelea kusoma unaona jinsi wana wa Yuda
hawakutaka kutii maagizo ya Mungu bali kufuata mambo ambayo waliyapokea kutoka
kwa mababu zao. Hayo mambo waliyapenda na
kuyaamini kuwa yanawasaidia na hivyo kupelekea hasira ya Mungu kuwaka katikati
yao na wao kupelekwa utumwani Babeli.
Mungu akawaambia nitawapa uhuru wa kuteswa na mataifa
utumwani. Kumbe Yuda walikuwa na ulinzi wa kimungu juu yao ya kuweza kuzuia
watu wasiwatese au kuwaonea. Lakini Mungu akaiondoa wakabaki wenyewe bila ulinzi na hivyo
wakateseka kwa mapigo mbalimbali.
Je wewe unateseka na mambo gani katika maisha yako? Umewahi
kujiuliza kama bado una ulinzi wa kimungu au umeshatoweka? Mara nyingi kukataa
maagizo ya Mungu kunapelekea kuondolewa ulinzi katika maeneo ya maisha yako.
Unatakiwa kujichunguza na kujihoji kama unafuata kwa uaminifu maagizo yote
yaliyoagizwa kwenye neno la Mungu.
Vitu tunavyoagizwa na Mungu kupitia neno lake ni kupendana, kusameheana, kuinuana, kutoa zaka
na sadaka mbalimbali, kusaidia wasiojiweza, kumsifu na kumuabudu, kuishi maisha
matakatifu nk.
Ni vizuri kuyafanya haya yote kwa uaminifu. Mtumie Roho mtakatifu
nae atakuwezesha kufanya haya. Pia jitahidi kusoma neno la Mungu kwani ndilo
uzima na litakuwezesha kujua nini cha kufanya na kwa namna gani. Kumbuka hakuna
kinachoshindikana kwa Bwana kama ukiamua na kuamini.
Utii ni Bora kuliko sadaka, kwahiyo nivema ukatii maagizo ya
Mungu na hapo ndipo utakapokua chini ya ulinzi wa Mungu katika kuingia kwako na
kutoka kwako, na shetani hatapata nafasi katika maisha yako.
Matatizo mengi huja kwa kuachwa mlango wazi katika maisha yako. Funga milango
yako yote ili shetani asipate nafasi. Funga milango ya
uongo, uvivu, wivu, masengenyo, ulafi, uzinzi, ufisadi, kuabudu/kutegemea miungu mingine n.k. uone kama utaonewa
tena na shetani. Hakika hatapata nafasi.
Usiwe kama wana wa Israeli ambao hawakutii maagizo ya Mungu,
na mabaya yakawapata. Anza kutii maagizo ya Mungu leo uishi katika ulinzi
wake.
karibu tujifunze neno
ReplyDelete