Friday, 31 March 2017

Unaweza kupata unachokitaka kutoka kwa Mungu



Habari msomaji wangu,
Karibu kwenye somo la leo.

Tunamtumikia Mungu mkuu na mwenye upendo. Ni maombi yangu kwako kuwa wewe na wale wote wanaokuzunguka muweze kujua na kuishi upendo wa Mungu na ukuu wake kwa kiasi kikubwa kuliko hapo mwanzo.

Lakini ngoja nikuulize kitu: Je unayo imani ya kuweza kuamini mambo makuu ya Mungu katika maisha yako?

Neno la Mungu linasema Mungu yuko kwa ajili ya kukuongeza na kukufanya usonge mbele, Mungu huwa harudi nyuma. Tunasoma kwenye Hagai 2:9,  “Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza.”  Hii  ina maana kuwa Mungu hayuko katika kurudia kitu alicho kifanya bali kufanya vizuri zaidi na kwa upya, na ataenda kufanya kitu kikubwa zaidi kwako Haleluya!

Yesu alisema wale wote watakaomuamini watafanya mambo makubwa zaidi ya yale aliyoyafanya yeye Yesu (Yohana 14:12).

Nimegundua ya kuwa imani na matarajio yanakwenda pamoja. Kama mtu anasema anayo imani juu ya kitu fulani halafu mwenendo wake hauonekani kukitarajia hicho kitu kutokea, hiyo inakuwa ni kama kufikirika tu (wish) na siyo imani.

Natamani kwa ujumbe huu ukaimarishe imani yako ambayo itazaa matarajio katika maisha yako ili kuona na kuishi mambo makubwa ambayo Mungu wetu anayo kwa ajili ya maisha yako.

Je unaamani kabisa kuwa Mungu anacho kitu kizuri na kikubwa kwa ajili ya kazi yako, ndoa yako, watoto wako fedha zako, utumishi wako na mambo yote katika maisha yako? Kama ndiyo, basi tarajia kuwa itakuja kuwa halisi katika maisha yako.
Yesu alisema “ Je unaamini ya kuwa ninaweza kukufanyia haya?..... Kutokana na imani yako pokea “ ( Mathayo 9:28-29).

Imani na matarajio huenda pamoja. Ila haitaishia hapo. Kama kweli unaamini, na unajua itakuja kutokea, basi tutaona kwa namna unavyoongea na kuishi

Najua kuna watu ambao wanafikiri kusema au kukiri kitu hakina uhusiano na kupokea hicho kitu. Kama ukitamka na kuweka maneno unayotamka katika imani na matarajio, utakuwa unatengeneza mazingira ya Mungu kukufanyia au kukupa hicho kitu katika maisha yako, na tena kwa haraka zaidi kama hutakata tamaa. Hii ndiyo njia ya kibiblia ya kupata vitu vyako unavyovihitaji.

Kuna laana na uzima katika kuongea (Mithali 18:21). Unaweza ukaona hili neno likifanya kazi kuanzia agano la kale, agano jipya na hata katika maisha yetu ya kawaida.

Mtume Paulo anatuambia kwenye Warumi 4:17 yakuwa Mungu alimuita Abram kuwa Abraham kwasababu yeye atakuwa Baba wa Mataifa mengi. Hapa tunaona Mungu alimuita Abraham baba wa mataifa mengi wakati Abraham alikuwa hana hata mtoto mmoja, na mke wake Sara alikuwa tasa na mwenye umri mkubwa. Embu angalia mazingira aliyokuwa nayo Abraham na mkewe yalikuwa ni magumu kwa macho ya kibinadamu. Ni kitu ambacho hakiwezekani lakini Mungu aliamua kutamka hivyohivyo.

Je wewe uko na mazingira gani ambayo unaona magumu na haiwezeni kupata unachokitamani? Embu amua kutamka na kuamini ya kuwa kitawezekana leo na uanze kukiishi hatakama hakijatokea bado haleluya! Kwasababu tumeambiwa kwa kadiri ya imani yetu tutapokea kutoka kwa Mungu.
Tunaona nguvu ya kutamka kitu unachokihitaji ni muhimu sana. Na siyo kutamka mara moja tu, fanya hivyo kila siku. Na ukitaka iwe rahisi kwako kufanya hivyo, hakikisha unachapa hilo hitaji lako kwenye karatasi au andika kwa mkono kwenye karatasi, halafu ibandike kwenye ukuta wako wa chumbani,  ofisini, kwenye computer yako kwenye wallet yako nk. Hii itakusaidia ukiwa popote unaweza kuisoma na inakukumbusha kuwa unakitu unakitarajia kutoka kwa Bwana.
Tumeona hapo kwenye warumi 4:17. Mungu alikuwa anatamani kuona Abraham akiwa ni baba wa mataifa mengi. Mungu hakuishia kutamani tu, bali alianza kuifanyia kazi imani yake kwa njia ya kimatendo kumbadilisha jina Abram kuwa Abraham. Hiki kitendo ndicho kile tunasema kuiishi imani. Yaani unaanza kuanda mazingira ya kupokea muujiza wako.

Mtume Paulo anatuambia tunayo roho ileile ya imani kama Baba yetu wa mbinguni (2 Wakorintho 4:13). Usiruhusu mazingira yako yakufanye uongee unachokiona kwa wakati huo. Anza kusema “mambo makubwa yasiyoonekana yanakwenda kutokea katika maisha yangu, Baraka za Mungu, na kufunguliwa kwangu kunakwenda kutokea”.
Hivi ndivyo  ninafanya katika maisha yangu na ninaona mambo makubwa yakinitokea pale ambapo palikuwa panaonekana haiwezekani kabisa, naona Mungu akifanya.   

Kila mara ninapokwenda kusikiliza neno la Mungu natafuta ni nini Mungu anasema na ninalichukua na kulifanya la kwangu na kuanza kulitamkia na kuliishi kana kwamba nimelipata tayari. Na ndipo hilo neno huwa halisi katika maisha yangu.
Kuna ujumbe mwingi sana ambao wewe kama mkristo unaupata kwa kuhudhuria semina na makongamano mbalimbali na huko kote Mungu anakuwa na ujumbe mahususi kwa ajili ya tatizo au hitaji ulilonalo. Shida inakuwa ni pale hauko tayari kutafuta nini Mungu anasema nawewe ili uuchukue na kufanyia kazi kama nilivyoelezea. Mara nyingi unasifia tu ujumbe ni mzuri lakini wewe huchukui hatua ya kuufanya ujumbe uwe wa kwako na kuunenea kila siku na kuishi kama vile umeshakuwa halisi.

Mpendwa msomaji wangu. Tunaambiwa ya kuwa tunaangamia kwa kukosa maarifa. Embu pata maarifa leo na uanze kubadilisha maisha yako. Chukua hili kama desa lako. Copy na upaste kwenye maisha yako na uone jinsi utakavyo anza kuishi kwa ubora zaidi kuliko hapo mwanzo.

2 comments:

  1. Mithali 8:11 nawapenda wale wanipendao na wale wanitaftao kwa bibi watanionaa. Mungu anatukumbusha kwa BIDII...
    mungu atusaidie tuzidi kumtafta kwa bidii ili ashughulike zaidi na mahitaji yetu kwani amesema leteni aja zenu....

    ReplyDelete
  2. Bidii ni muhimu kwa ajili ya kuweza kupata kutoka kwa Bwana

    ReplyDelete