Habari msomaji wangu,
Karibu kwenye somo la leo.
Tunamtumikia Mungu mkuu na mwenye upendo. Ni maombi yangu
kwako kuwa wewe na wale wote wanaokuzunguka muweze kujua na kuishi upendo wa
Mungu na ukuu wake kwa kiasi kikubwa kuliko hapo mwanzo.
Lakini ngoja nikuulize kitu: Je unayo imani ya kuweza
kuamini mambo makuu ya Mungu katika maisha yako?
Neno la Mungu linasema Mungu yuko kwa ajili ya kukuongeza na
kukufanya usonge mbele, Mungu huwa harudi nyuma. Tunasoma kwenye Hagai
2:9, “Utukufu wa mwisho wa nyumba hii
utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza.” Hii ina
maana kuwa Mungu hayuko katika kurudia kitu alicho kifanya bali kufanya vizuri
zaidi na kwa upya, na ataenda kufanya kitu kikubwa zaidi kwako Haleluya!
Yesu alisema wale wote watakaomuamini watafanya mambo
makubwa zaidi ya yale aliyoyafanya yeye Yesu (Yohana 14:12).
Nimegundua ya kuwa imani
na matarajio yanakwenda pamoja. Kama
mtu anasema anayo imani juu ya kitu fulani halafu mwenendo wake hauonekani
kukitarajia hicho kitu kutokea, hiyo inakuwa ni kama kufikirika tu (wish) na
siyo imani.
Natamani kwa ujumbe huu ukaimarishe imani yako ambayo itazaa
matarajio katika maisha yako ili kuona na kuishi mambo makubwa ambayo Mungu
wetu anayo kwa ajili ya maisha yako.
Je unaamani kabisa kuwa Mungu anacho kitu kizuri na kikubwa
kwa ajili ya kazi yako, ndoa yako, watoto wako fedha zako, utumishi wako na
mambo yote katika maisha yako? Kama ndiyo, basi tarajia kuwa itakuja kuwa halisi katika maisha yako.
Yesu alisema “ Je unaamini ya kuwa ninaweza
kukufanyia haya?..... Kutokana na imani yako pokea “ ( Mathayo 9:28-29).
Imani na matarajio huenda pamoja. Ila haitaishia hapo. Kama
kweli unaamini, na unajua itakuja kutokea, basi tutaona kwa namna unavyoongea na kuishi.
Najua kuna watu ambao wanafikiri kusema au kukiri kitu
hakina uhusiano na kupokea hicho kitu. Kama ukitamka na kuweka maneno
unayotamka katika imani na matarajio, utakuwa unatengeneza mazingira ya Mungu
kukufanyia au kukupa hicho kitu katika maisha yako, na tena kwa haraka zaidi
kama hutakata tamaa. Hii ndiyo njia ya kibiblia ya kupata vitu vyako
unavyovihitaji.
Kuna laana na uzima katika kuongea (Mithali 18:21). Unaweza
ukaona hili neno likifanya kazi kuanzia agano la kale, agano jipya na hata
katika maisha yetu ya kawaida.
Mtume Paulo anatuambia kwenye Warumi 4:17 yakuwa Mungu
alimuita Abram kuwa Abraham kwasababu yeye atakuwa Baba wa Mataifa mengi. Hapa
tunaona Mungu alimuita Abraham baba wa mataifa mengi wakati Abraham alikuwa
hana hata mtoto mmoja, na mke wake Sara alikuwa tasa na mwenye umri mkubwa. Embu
angalia mazingira aliyokuwa nayo Abraham na mkewe yalikuwa ni magumu kwa macho
ya kibinadamu. Ni kitu ambacho hakiwezekani lakini Mungu aliamua kutamka
hivyohivyo.
Je wewe uko na mazingira gani ambayo unaona magumu na
haiwezeni kupata unachokitamani? Embu amua kutamka na kuamini ya kuwa
kitawezekana leo na uanze kukiishi hatakama hakijatokea bado haleluya!
Kwasababu tumeambiwa kwa kadiri ya imani yetu tutapokea kutoka kwa Mungu.
Tunaona nguvu ya kutamka kitu unachokihitaji ni muhimu sana.
Na siyo kutamka mara moja tu, fanya hivyo kila siku. Na ukitaka iwe rahisi
kwako kufanya hivyo, hakikisha unachapa hilo hitaji lako kwenye karatasi au
andika kwa mkono kwenye karatasi, halafu ibandike kwenye ukuta wako wa chumbani,
ofisini, kwenye computer yako kwenye
wallet yako nk. Hii itakusaidia ukiwa popote unaweza kuisoma na inakukumbusha
kuwa unakitu unakitarajia kutoka kwa Bwana.
Tumeona hapo kwenye warumi 4:17. Mungu alikuwa anatamani
kuona Abraham akiwa ni baba wa mataifa mengi. Mungu hakuishia kutamani tu, bali
alianza kuifanyia kazi imani yake kwa njia ya kimatendo kumbadilisha jina Abram
kuwa Abraham. Hiki kitendo ndicho kile tunasema kuiishi imani. Yaani unaanza
kuanda mazingira ya kupokea muujiza wako.
Mtume Paulo anatuambia tunayo roho ileile ya imani kama Baba
yetu wa mbinguni (2 Wakorintho 4:13). Usiruhusu mazingira yako yakufanye uongee
unachokiona kwa wakati huo. Anza kusema “mambo makubwa yasiyoonekana yanakwenda
kutokea katika maisha yangu, Baraka za Mungu, na kufunguliwa kwangu kunakwenda
kutokea”.
Hivi ndivyo ninafanya
katika maisha yangu na ninaona mambo makubwa yakinitokea pale ambapo palikuwa
panaonekana haiwezekani kabisa, naona Mungu akifanya.
Kila mara ninapokwenda kusikiliza neno la Mungu natafuta ni nini
Mungu anasema na ninalichukua na kulifanya la kwangu na kuanza kulitamkia na
kuliishi kana kwamba nimelipata tayari. Na ndipo hilo neno huwa halisi katika
maisha yangu.
Kuna ujumbe mwingi sana ambao wewe kama mkristo unaupata kwa
kuhudhuria semina na makongamano mbalimbali na huko kote Mungu anakuwa na
ujumbe mahususi kwa ajili ya tatizo au hitaji ulilonalo. Shida inakuwa ni pale
hauko tayari kutafuta nini Mungu anasema nawewe ili uuchukue na kufanyia kazi kama
nilivyoelezea. Mara nyingi unasifia tu ujumbe ni mzuri lakini wewe huchukui
hatua ya kuufanya ujumbe uwe wa kwako na kuunenea kila siku na kuishi kama vile
umeshakuwa halisi.
Mpendwa msomaji wangu. Tunaambiwa ya kuwa tunaangamia kwa
kukosa maarifa. Embu pata maarifa leo na uanze kubadilisha maisha yako. Chukua
hili kama desa lako. Copy na upaste kwenye maisha yako na uone jinsi utakavyo
anza kuishi kwa ubora zaidi kuliko hapo mwanzo.