Yohana 4:23
“Lakini saa inakuja, nayo saa ipo ambayo waabuduo halisi
watamwabudu Baba katila roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao
wamwabudu.”
Katika mstari huu tunaweza kuona ya kuwa kuna waabudio
halisi. Na kama kuna waabudio halisi pia kutakuwa na waabudio wasio halisi. Pia
inasema waabudio halisi ni wachache na ndiyo maana Baba anawatafuta hao ili
wamwabudu.
Je ni kwa namna gani unaweza kumwabudu Mungu?
Ni kwa kuishi maisha ya rohoni katika kila nyanja ya maisha
yako. Iwe kwa kusema kwako, kwa kutenda kwako na kutembea kwako.
Kuabudu anakokutaka Mungu Baba ni kule kunakotoka katika roho yako na siyo katika nafsi yako.
Tofauti ni kuwa, kwenye nafsi yako ndiko kunakotoka kufikiri kwako na kuona
mantiki ya kitu kutokana na mazingira yanayokuzunguka, watu wanavyosema au wewe
unavyojisikia.
Kwenye roho yako ni mahali ambapo ni pa ukweli unaotokana na
neno la Mungu, roho huangalia neno na si mazingira. Ndiyo maana hata ukiwa
katika taabu unatakiwa ufurahie kwasababu neno linasema hivyo. Kwenye roho
hakuna kikomo ni utimilifu tu na ukiamini na kuishi katika roho, hakika utakuwa
ni mtu wa kuishi maisha ya ushindi tu kila siku.
Utajuaje kama unamuabudu Mungu katika roho na kweli au la.
Mtu asiyemwabudu Mungu katika roho anakuwa anaabudu kutokana
na mazingira yanayomzunguka. Mfano umefaulu shule ndipo unamuabudu
kwasababu hiyo, au unauchungu fulani ndipo unaingia kumuabudu Mungu kutokana na
hisia ulizonazo na kulia kwa uchungu.
Mara nyingi hata nyimbo za kuabudu unakuta
zinaimbwa lakini maneno yake unakuta yanatuongelea sisi na maisha yetu badala ya kumuongelea Mungu na uweza wake. Kwahiyo unakuta mtu
anavuta hisia ya vitu vinavyomzunguka na kupata msisimko akifikiri anamuabudu
Mungu kumbe la hasha.
Kumuabudu Mungu katika roho na kweli siyo tukio (event),
bali ni maisha ya kila siku na kila wakati. Hii ina maana unamwabudu Mungu kwa
jinsi alivyo yeye pekee, uweza wake, ukuu wake, bila kuruhusu akili yako
kusikiliza hisia zinazokuzunguka.
Tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kumwabudu Mungu katika
roho na kweli ambapo tutamuangalia yeye tu na uweza wake pasipo kuangalia
magumu yaliyotuzunguka.