Sunday, 9 July 2017

Kinywa chako, maisha yako


Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake. Mithali 12:14

Chochote mtu atakachokuwa anatamka katika kinywa chake ndicho atakifanya kiwe kama alivyotamka. Ni vema kutamka mema kwako na kwa wengine. Hata siku moja usikubali kutamka neno ovu ama linaloonyesha udhaifu fulani katika maisha yako na ya wengine. Kwasababu, kwa kutamka maneno unayapa uwezo wa kufuatiliwa na nguvu iliyoko nyuma ya hayo maneneo na kuleta sawasawa na hiyo nguvu ilivyotafsiriwa na ubongo wako.

Anza leo kufuta maneno yote hasi  uliyowahi kutamka kwako mwenyewe na kwa wengine. Anza leo kutamka maneno chanya yenye kuleta amani na ushindi juu ya maisha yako na ya wengine pia.

Kwa mfano: Usiseme "Sitaki kufeli"
                     Sema " Nataka kufaulu"

Jua ya kuwa, ukisema sitaki kufeli, kuna nguvu ambayo inaambatana na hilo neno ambalo ni nguvu hasi yenye kuleta hofu. Hofu ya kufeli. Kwahiyo hatakama hutaki kufeli, maadamu umeshataja kufeli, hiyo nguvu huambatana na neno na kukupa hilo hitaji la kufeli.

Ukisema nataka kufaulu, vivo hivyo kuna nguvu nyuma ya hilo neno. Nguvu chanya ya ushindi ambayo itakupelekea kushinda. 

Kumbe maneno nayo yana nguvu nyuma yake ya kupelekea ubongo (subconcious) ifanye kama inavyojisikia kutokana na nguvu iletayo hisia (emotions) zilizojengeka wakati wa kutamka hayo maneno.

Hivyo basi ili kuweza kupata hitaji lako, unatakiwa 
  1. Ulifikirie (think about it)
  2. Ulitamke kwa mtazamo chanya (speak out loud)
  3. Weka hisia (emotions) hapa ni hali utakavyojisikia kama vile umeshalipata hitaji lako.
  4. Lipokee (receive)
  5. Litakuwa lako (will be yours)

Wednesday, 24 May 2017

Kumwabudu Mungu katika roho na kweli



Yohana 4:23
“Lakini saa inakuja, nayo saa ipo ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katila roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”

Katika mstari huu tunaweza kuona ya kuwa kuna waabudio halisi. Na kama kuna waabudio halisi pia kutakuwa na waabudio wasio halisi. Pia inasema waabudio halisi ni wachache na ndiyo maana Baba anawatafuta hao ili wamwabudu.

Je ni kwa namna gani unaweza kumwabudu Mungu?

Ni kwa kuishi maisha ya rohoni katika kila nyanja ya maisha yako. Iwe kwa kusema kwako, kwa kutenda kwako na kutembea kwako.
Kuabudu anakokutaka Mungu Baba ni kule kunakotoka katika roho yako na siyo katika nafsi yako. Tofauti ni kuwa, kwenye nafsi yako ndiko kunakotoka kufikiri kwako na kuona mantiki ya kitu kutokana na mazingira yanayokuzunguka, watu wanavyosema au wewe unavyojisikia.

Kwenye roho yako ni mahali ambapo ni pa ukweli unaotokana na neno la Mungu, roho huangalia neno na si mazingira. Ndiyo maana hata ukiwa katika taabu unatakiwa ufurahie kwasababu neno linasema hivyo. Kwenye roho hakuna kikomo ni utimilifu tu na ukiamini na kuishi katika roho, hakika utakuwa ni mtu wa kuishi maisha ya ushindi tu kila siku.

Utajuaje kama unamuabudu Mungu katika roho na kweli au la.

Mtu asiyemwabudu Mungu katika roho anakuwa anaabudu kutokana na mazingira yanayomzunguka. Mfano umefaulu shule ndipo unamuabudu kwasababu hiyo, au unauchungu fulani ndipo unaingia kumuabudu Mungu kutokana na hisia ulizonazo na kulia kwa uchungu.



Mara nyingi hata nyimbo za kuabudu unakuta zinaimbwa lakini maneno yake unakuta yanatuongelea sisi na maisha yetu badala ya kumuongelea Mungu na uweza wake. Kwahiyo unakuta mtu anavuta hisia ya vitu vinavyomzunguka na kupata msisimko akifikiri anamuabudu Mungu kumbe la hasha.

Kumuabudu Mungu katika roho na kweli siyo tukio (event), bali ni maisha ya kila siku na kila wakati. Hii ina maana unamwabudu Mungu kwa jinsi alivyo yeye pekee, uweza wake, ukuu wake, bila kuruhusu akili yako kusikiliza hisia zinazokuzunguka.


Tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kumwabudu Mungu katika roho na kweli ambapo tutamuangalia yeye tu na uweza wake pasipo kuangalia magumu yaliyotuzunguka.

Kuwekwa huru mbali na sheria ya dhambi



Warumi 8:1-2
“Sasa basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwasababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.”

Hii ni kwa namna gani?
Kipindi kile cha sheria ya Musa, watu walikuwa wanaishi kutegemea mwili na si rohoni. Mwili ni dhaifu kwa habari ya kufuata sheria za Mungu. Hii ilitokana na laana ya dhambi iliyofanyika pale katika bustani ya Edeni ambapo Eva alidanganywa na nyoka na kula tunda alilokatazwa na Mungu. Walipoondolewa kutoka bustanini, utawala wote waliokuwa nao Adam na Eva uliingia mikononi mwa shetani ambaye ni mleta laana.

Hata sheria ya Mungu iliyoletwa na Musa ilipokuja, kwasababu ya laana, watu  hawakuweza kuitimiza sheria. Watu walibaki wakiwa wanahukumiwa kwasababu ya dhambi zao na kuishi maisha ya kushindwa kila wakati.

Ashukuriwe Mungu mwenyenzi kumleta Yesu Kristo mwanane na kuja kufa kwa ajili yetu na kuondoa sheria ya dhambi na mauti iliyoletwa na shetani, na kuweka sheria ya uzima ndani ya kila atakaye muamini. Ukiamua kumwamini Kristo Yesu, basi hakutakuwa na hukumu ya dhambi na mauti juu yako kwasababu sheria ya roho wa uzima inakuweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. Na hii inawezekana kwasababu wewe utakuwa hauenendi tena katika mwili ambao ni dhaifu kupokea sheria za Mungu, bali uko katika roho ambamo sheria ya Mungu inawekwa ndani yako automatically, wala hutakuwa na haja ya kutumia nguvu kuacha dhambi. Utajikuta tu unajua hii ni dhambi na hivyo utaachana nayo au utakaa mbali nayo.

Mpendwa msomaji ukiona bado unatumia nguvu sana kuacha dhambi na kwa muda mrefu, nakusihi ujichunguze kwa habari ya wokovu wako kwasababu hutakiwi kuishi na tamaa za mwili wakati unatakiwa kutawaliwa na Roho Mtakatifu ili akuweke huru mbali na dhambi na mauti.

Thursday, 4 May 2017

Namna ya kumlilia Mungu katika shida yako



Zaburi 107:19-20 inasema “Wakamlilia Bwana katika shida zao. Akawaponya na shida zao.Hulituma neno lake huwaponya. Huwatoa katika maangamizi”

Ashukuriwe Mungu aliye juu kwakuwa tunalo tumaini katika yeye. Kwakuwa ndiye ngome yetu na msaada wetu wakati wa mateso.

Leo ningependa nikukumbushe kwa habari ya kumlilia Mungu katika shida uliyonayo.Kwa maana imeandikwa muite Mungu maadamu anapatikana.

Mara nyingi tunakuwa katika shida na taabu katika maisha yetu na tunakaa hapo hapo katika hiyo shida kwa muda mrefu sana kuliko ilivyotakiwa. Ni kwanini? Hii ni kwasababu hatumlilii Mungu katika shida zetu. Unaweza kujiuliza mbona huwa ninaomba sana lakini majibu hayaji. Hii pia ni kwasababu unaomba vibaya. Imeandikwa kuwa” hampati kwasababu mnaomba vibaya”.

Kuomba vibaya ni kwa namna gani?
Ni kwa kulalamika na kuliangalia tatizo lako zaidi ya kumuangalia Mungu na uweza wake wa kuliondoa tatizo. Mara nyingi unakuwa na maombi yanayotokana katika nafsi yako kuliko yanayotoka rohoni. Rohoni ni mahali pasipo na waa na ndipo Mungu hukaa. Kwenye nafsi yako ni mahali unafanya maamuzi kutokana na hali halisi inayokuzunguka. Hivyo kuomba vizuri ni kuomba sawasawa na neno la Mungu, na si mapenzi yako.
Tukiweza kuomba sawasawa na neno lake, atasikia. Mara kwa mara tunaomba sawasawa na mapenzi yetu, na ndipo Mungu hatusikiii kwasabau hujaingia bado kwenye himaya yake. Kulia sana na uchungu sana hausaidii na tena imeandikwa “uchungu wote na uondoke kwenu.”

Embu chunguza hayo unayomuomba Mungu na namna unavyomuomba, je unaomba kwa hisia ya mwilini au katika roho? Mungu ni roho, ukitaka kuongea nae uwe katika roho na ndipo Roho Mtakatifu hutusaidia pale tunaposhindwa kuomba katika roho.

Nakusihi uanze kutafuta kujua namna ya kumuomba Mungu katika roho na utaona jinsi majibu utakavyoyapata kwa haraka kama neno linavyosema walimlilia, wakaponywa na kuondolewa katika maangamizi yao.

Mungu yuko tayari kukupa hitaji lako unalomuomba, ni wewe ambaye unachelewa kujua mapenzi yake ili uweze kupata haja za moyo wako.

Monday, 24 April 2017

Ulimwengu haututambui




Karibu kwenye somo la leo.

1 Yohana 3: 1 inasema “Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwasababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.”

Ni jambo la kushukuru sana kuitwa mtoto wa mtu mkubwa, maarufu na mwenye utajiri mwingi hapa duniani.  Na hii ni kwasababu unajua ya kuwa matatizo  utakayoyapata yatatatuliwa kwa haraka na bila shaka kabisa. Mtu mwenye uwezo wa kifedha na  maarifa ni mtu anayeweza kutatua changamoto zake kwa uraisi zaidi kuliko mtu asiye na fedha na maarifa. Ndiyo maana watoto wa matajiri wanakuwa na hali nzuri zaidi kimaisha kuliko watoto wa masikini.

Tukiangalia neno letu la leo tunaona ya kuwa tumeitwa wana wa Mungu na ndivyo tulivyo kama ilivyoandikwa pia kwenye  Yohana 1: 12 inayosema “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” Wewe kama umempokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, ujue tayari wewe ni mtoto wa Mungu.

Naomba tumuangalie huyu Mungu wetu alivyo ili tuweze kujua ni kwa namna gani wewe kama mtoto wake unatakiwa kuishi hapa duniani.
Mungu wetu ni mwenye uweza wote, ndiye aliyeziumba mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Ndiye mwenye kusamehe dhambi, Mungu ndiye mwenye dhahabu zote na fedha zote. Mungu anawalinzi ambao ni malaika wanaotulinda na kutuletea haja zetu usiku na mchana. Mungu ndiye mwenye kutupa pumzi ya uhai ili tuishi. Mungu hashindwi na lolote. Mungu ndiye mwenye mipango yako yote na ndiye mwenye kujua kila kitu katika maisha yako. Ukiomba chochote kwa Mungu sawasawa na mapenzi yake anakupa.

Mpendwa msomaji wangu, hivi kama huyu ndiye Mungu ambaye ni baba yako na  wewe ni mtoto wake, umesha wahi kujiuliza mbona maisha yako hayafanani na uweza wake?  Huenda tatizo ni sisi wenyewe kwa kutokumjua vizuri Mungu wetu na anataka nini kwetu.
Mara nyingi sisi tulioitwa watoto wa Mungu tunaishi maisha ambayo yanamichanganyo. Kwa Mungu kidogo, na kwa dunia kidogo. Tumeona katika hili neno  ya kuwa dunia haiwatambui wana wa Mungu, kwasababu hawakumtambua Mungu. Hii ina maana gani? Ukiwa kama mwana wa Mungu ni lazima utakuwa tofauti na dunia, kwa kuvaa, muonekano, kuongea na hata namna unavyoishi. Na kwasababu ya tofauti hizo, dunia inashindwa kukuelewa kwasababu vile vitu ambavyo wao wanavikimbilia, wewe huvikimbilii. Kama wewe ni makini wa kufuatilia maneno ya Mungu, utagundua vitu vingi ambavyo vinaendelea duniani ni kutoka kwa yule mwovu.

Tuangalie mfano mmoja wa mavazi, watu wa Mungu ambao ni kanisa lake kuna namna ambayo wanatakiwa kuonekana kama vile wanawake wasivae nguo fupi au wasivae suruale, na pia wasijipambe kwa dhahabu na kusuka nywele za bandia na mapambo ya  usoni (cosmetics). Haya yote yanaitwa ni machukizo mbele ya Mungu ambaye ni baba yetu. Kama wewe bado unafanya mambo kama hayo, ujue unamchukiza baba yako na unafanya mambo ambayo ni ya kidunia na kuacha mpango mzima wa Mungu katika maisha yako.

Mungu wetu anataka tuwe safi bila mawaa katika maisha yetu na siyo michanganyo ambayo mwishowe atakutapika siku zijazo.
Je wewe ni mwana wa Mungu nabado uko katika michanganyo hii ya dunia? Huenda ndiyo maana mambo yako hayaendi na kila ukiomba unaona kama unagonga mwamba. Ondoa unajisi katika maisha yako na uone jinsi Mungu ambaye ni baba yako wa mbinguni atakavyoshuka na kukuhudumia. Usimpe shetani nafasi kwa chochote katika maisha yako.

Soma zaidi maandiko yafuatayo kuhusu namna Mungu anavyopenda uwe na utagundua kumbe ni kinyume kabisa na namna dunia inavyotaka uwe.
1Wakorintho 14:34-35, 1Wakorintho 11:1-15, 1Timothy 2: 8-15, 1 Petro 3:3-5

Thursday, 6 April 2017

Utii ni bora kuliko sadaka



Habari msomaji wangu,

Karibu kwenye somo la leo.
Tunasoma kutoka kitabu cha Yeremia 34 kinachoongelea jinsi Mungu mwenyenzi alipoongea na nabii Yeremia na kumpa maagizo yake ili awaambie watu wa Yuda wakaao Israeli nini Mungu anapenda wafanye.

Lakini ukiendelea kusoma unaona jinsi wana wa Yuda hawakutaka kutii maagizo ya Mungu bali kufuata mambo ambayo waliyapokea kutoka kwa mababu zao. Hayo mambo  waliyapenda na kuyaamini kuwa yanawasaidia na hivyo kupelekea hasira ya Mungu kuwaka katikati yao na wao kupelekwa utumwani Babeli.

Mungu akawaambia nitawapa uhuru wa kuteswa na mataifa utumwani. Kumbe Yuda walikuwa na ulinzi wa kimungu juu yao ya kuweza kuzuia watu wasiwatese au kuwaonea. Lakini Mungu akaiondoa wakabaki wenyewe bila ulinzi na hivyo wakateseka kwa mapigo mbalimbali.

Je wewe unateseka na mambo gani katika maisha yako? Umewahi kujiuliza kama bado una ulinzi wa kimungu au umeshatoweka? Mara nyingi kukataa maagizo ya Mungu kunapelekea kuondolewa ulinzi katika maeneo ya maisha yako. Unatakiwa kujichunguza na kujihoji kama unafuata kwa uaminifu maagizo yote yaliyoagizwa kwenye neno la Mungu.

Vitu tunavyoagizwa na Mungu kupitia neno lake ni  kupendana, kusameheana, kuinuana, kutoa zaka na sadaka mbalimbali, kusaidia wasiojiweza, kumsifu na kumuabudu, kuishi maisha matakatifu nk.
Ni vizuri kuyafanya haya yote kwa uaminifu. Mtumie Roho mtakatifu nae atakuwezesha kufanya haya. Pia jitahidi kusoma neno la Mungu kwani ndilo uzima na litakuwezesha kujua nini cha kufanya na kwa namna gani. Kumbuka hakuna kinachoshindikana kwa Bwana kama ukiamua na kuamini.

Utii ni Bora kuliko sadaka, kwahiyo nivema ukatii maagizo ya Mungu na hapo ndipo utakapokua chini ya ulinzi wa Mungu katika kuingia kwako na kutoka kwako, na shetani hatapata nafasi katika maisha yako.

Matatizo mengi huja kwa kuachwa mlango wazi katika maisha yako. Funga milango yako yote ili shetani asipate nafasi. Funga milango ya uongo, uvivu, wivu, masengenyo, ulafi, uzinzi, ufisadi, kuabudu/kutegemea miungu mingine n.k. uone kama utaonewa tena na shetani. Hakika hatapata nafasi.

Usiwe kama wana wa Israeli ambao hawakutii maagizo ya Mungu, na mabaya yakawapata. Anza kutii maagizo ya Mungu leo uishi katika ulinzi wake.