Sunday, 4 February 2018

Maisha Ya Amani

Karibu msomaji wangu

Leo tunajifunza kuhusu AMANI.

Nini maana ya Amani. Amani ni ile hali ya kuishi bila wasiwasi au mashaka ya aina yoyote.
Amani ni hatua ya juu sana ya maisha ya mtu yenye kutamaniwa. Palipo na amani ndipo mtu anapenda kuishi hapo.

Ni namna gani mtu anaweza kuishi maisha ya Amani?
Ngoja tuone fomula ifuatayo ili kuweza kupata amani.

IMANI - HOFU = AMANI

Ndiyo, ukiwa na imani katika kitu fulani, halafu ukatoa hofu inayokuzunguka basi utakuwa na amani. Ukiifahamu hii fomula na kuifanyia kazi, itakusaidia kuvuka salama katika maeneo mengi unayoyapitia katika maisha yako.

Ukisoma Waebrania 11:1 inasema "Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana."
Ukiwa unaamini neno la Mungu kuhusu jambo fulani katika maisha yako, na ukiondoa hofu inayokuzungukia juu ya hilo jambo, utakuwa na Amani.

Hofu ni kule kuangalia hali inayokuzunguka na kukuogopesha. Inaweza kuwa ya wakati huohuo au ya kufikirika kwa wakati ujao.

Ili kuweza kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, usiwe mtu wa hofu. Ondoa hofu katika kila unalolifanya. Wewe amini tu kuwa unaweza au inawezekana kupona ugonjwa huo, kupata kazi nzuri, kupata ndoa nzuri, kupata watoto wema, kuwa mtu muhimu n.k. Hii ndiyo imani.

Usiangalie ni hali gani unayoipitia kwa sasa, bali macho yako yaone kile unachokiamini na ndipo utapata Amani na pole pole utaanza kuona kile kitu unachoamini kinatokea.

Mara zote hofu ndiyo inayokufanya usipige hatua, na unakuwa sikuzote mtu wa sintofahamu. Yaani sijui itakuwaje katika kila jambo. Ukiona hali hiyo ujue uko katika hofu.

Amua leo kuondoa hofu katika maisha yako na uamini kile alichosema Mungu kuwa utaweza na utapata. Hapo utaanza kuona maisha yako yanabadilika na kuwa ya Amani.


Wednesday, 17 January 2018

Mwanzo wa Mwaka mpya


Tunanamshukuru Mungu kwa kutuingiza kwenye mwaka mwingine mpya.
Mungu analo kusudi katika maisha yako, kwani hadi leo hii amekuweka hai ukiwa katika hali hiyo uliyonayo. Maadam uko hai, unayonafasi ya kufanya kitu cha tofauti katika maisha yako. Nina maana unao uwezo wa kubadilisha hali uliyonayo sasa ukaifanya ikawa bora zaidi.

Embu tuangalie maandiko, Waefeso 2:6 inasema "Akatufufua pamoja nae, akatuketisha pamoja nae katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu...."

Hapa tunaona ya kuwa baada ya wewe kumpokea Yesu Kristo, Yesu alikufufua na kukuweka katika ulimwengu wa roho. Hili ni neno linalotia hamasa sana yakuwa kumbe wewe sasa hivi uko katika ulimwengu wa roho. Na tunajua ya kuwa ukiwa katika ulimwengu wa roho unaouweza wa kufanya chochote utakacho kwasababu unakuwa hauna ukomo (limit)

Umeshawahi kusikia hata mapepo yanaweza kufanya chochote au kuingia popote bila shida, hii ni kwasababu wako katika ulimwengu wa roho. Mungu yuko katika ulimwengu wa roho na hata shetani pia yuko katika ulimwengu wa roho.

Ndugu yangu, ukiwa katika ulimwengu wa roho, unakuwa na uweza wa kutenda mambo.

Sasa umeshajua ya kuwa Yesu alikufufua pamoja nae na amekuketisha pamoja nae katika ulimwengu wa roho. Anza kuamini uko katika ulimwengu wa roho sasa, na anza kutumia mamlaka uliyonayo kwa kupitia neno la Mungu kuamuru vitu vinavyokuzunguka, kuumiza , shindikana, kufanyika kama unavyotaka wewe.

Uwezo unao na mamlaka unayo. Jifunze zaidi maneno ya Mungu ili uweze kujua namna unavyoweza kupata ushindi wakati huu na utaona utakavyobadilisha hali yako na maisha yako kwa urahisi kabisa.
Je ni ada ya mtoto hauna? Je ni kazi hauna? Je hujapata wa kukuoa? Je una ugonjwa unaokusumbua? Je una madeni yanayo kushinda kulipa? Je una kesi mahakamani? Yote hayo yako katika uwezo uliopewa na Mungu kwa kupitia Yesu Kristo. Acha kukata tamaa, anza leo kutumia mamlaka uliyonayo.

Sunday, 9 July 2017

Kinywa chako, maisha yako


Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake. Mithali 12:14

Chochote mtu atakachokuwa anatamka katika kinywa chake ndicho atakifanya kiwe kama alivyotamka. Ni vema kutamka mema kwako na kwa wengine. Hata siku moja usikubali kutamka neno ovu ama linaloonyesha udhaifu fulani katika maisha yako na ya wengine. Kwasababu, kwa kutamka maneno unayapa uwezo wa kufuatiliwa na nguvu iliyoko nyuma ya hayo maneneo na kuleta sawasawa na hiyo nguvu ilivyotafsiriwa na ubongo wako.

Anza leo kufuta maneno yote hasi  uliyowahi kutamka kwako mwenyewe na kwa wengine. Anza leo kutamka maneno chanya yenye kuleta amani na ushindi juu ya maisha yako na ya wengine pia.

Kwa mfano: Usiseme "Sitaki kufeli"
                     Sema " Nataka kufaulu"

Jua ya kuwa, ukisema sitaki kufeli, kuna nguvu ambayo inaambatana na hilo neno ambalo ni nguvu hasi yenye kuleta hofu. Hofu ya kufeli. Kwahiyo hatakama hutaki kufeli, maadamu umeshataja kufeli, hiyo nguvu huambatana na neno na kukupa hilo hitaji la kufeli.

Ukisema nataka kufaulu, vivo hivyo kuna nguvu nyuma ya hilo neno. Nguvu chanya ya ushindi ambayo itakupelekea kushinda. 

Kumbe maneno nayo yana nguvu nyuma yake ya kupelekea ubongo (subconcious) ifanye kama inavyojisikia kutokana na nguvu iletayo hisia (emotions) zilizojengeka wakati wa kutamka hayo maneno.

Hivyo basi ili kuweza kupata hitaji lako, unatakiwa 
  1. Ulifikirie (think about it)
  2. Ulitamke kwa mtazamo chanya (speak out loud)
  3. Weka hisia (emotions) hapa ni hali utakavyojisikia kama vile umeshalipata hitaji lako.
  4. Lipokee (receive)
  5. Litakuwa lako (will be yours)

Wednesday, 24 May 2017

Kumwabudu Mungu katika roho na kweli



Yohana 4:23
“Lakini saa inakuja, nayo saa ipo ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katila roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.”

Katika mstari huu tunaweza kuona ya kuwa kuna waabudio halisi. Na kama kuna waabudio halisi pia kutakuwa na waabudio wasio halisi. Pia inasema waabudio halisi ni wachache na ndiyo maana Baba anawatafuta hao ili wamwabudu.

Je ni kwa namna gani unaweza kumwabudu Mungu?

Ni kwa kuishi maisha ya rohoni katika kila nyanja ya maisha yako. Iwe kwa kusema kwako, kwa kutenda kwako na kutembea kwako.
Kuabudu anakokutaka Mungu Baba ni kule kunakotoka katika roho yako na siyo katika nafsi yako. Tofauti ni kuwa, kwenye nafsi yako ndiko kunakotoka kufikiri kwako na kuona mantiki ya kitu kutokana na mazingira yanayokuzunguka, watu wanavyosema au wewe unavyojisikia.

Kwenye roho yako ni mahali ambapo ni pa ukweli unaotokana na neno la Mungu, roho huangalia neno na si mazingira. Ndiyo maana hata ukiwa katika taabu unatakiwa ufurahie kwasababu neno linasema hivyo. Kwenye roho hakuna kikomo ni utimilifu tu na ukiamini na kuishi katika roho, hakika utakuwa ni mtu wa kuishi maisha ya ushindi tu kila siku.

Utajuaje kama unamuabudu Mungu katika roho na kweli au la.

Mtu asiyemwabudu Mungu katika roho anakuwa anaabudu kutokana na mazingira yanayomzunguka. Mfano umefaulu shule ndipo unamuabudu kwasababu hiyo, au unauchungu fulani ndipo unaingia kumuabudu Mungu kutokana na hisia ulizonazo na kulia kwa uchungu.



Mara nyingi hata nyimbo za kuabudu unakuta zinaimbwa lakini maneno yake unakuta yanatuongelea sisi na maisha yetu badala ya kumuongelea Mungu na uweza wake. Kwahiyo unakuta mtu anavuta hisia ya vitu vinavyomzunguka na kupata msisimko akifikiri anamuabudu Mungu kumbe la hasha.

Kumuabudu Mungu katika roho na kweli siyo tukio (event), bali ni maisha ya kila siku na kila wakati. Hii ina maana unamwabudu Mungu kwa jinsi alivyo yeye pekee, uweza wake, ukuu wake, bila kuruhusu akili yako kusikiliza hisia zinazokuzunguka.


Tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kumwabudu Mungu katika roho na kweli ambapo tutamuangalia yeye tu na uweza wake pasipo kuangalia magumu yaliyotuzunguka.

Kuwekwa huru mbali na sheria ya dhambi



Warumi 8:1-2
“Sasa basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwasababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru mbali na sheria ya dhambi na mauti.”

Hii ni kwa namna gani?
Kipindi kile cha sheria ya Musa, watu walikuwa wanaishi kutegemea mwili na si rohoni. Mwili ni dhaifu kwa habari ya kufuata sheria za Mungu. Hii ilitokana na laana ya dhambi iliyofanyika pale katika bustani ya Edeni ambapo Eva alidanganywa na nyoka na kula tunda alilokatazwa na Mungu. Walipoondolewa kutoka bustanini, utawala wote waliokuwa nao Adam na Eva uliingia mikononi mwa shetani ambaye ni mleta laana.

Hata sheria ya Mungu iliyoletwa na Musa ilipokuja, kwasababu ya laana, watu  hawakuweza kuitimiza sheria. Watu walibaki wakiwa wanahukumiwa kwasababu ya dhambi zao na kuishi maisha ya kushindwa kila wakati.

Ashukuriwe Mungu mwenyenzi kumleta Yesu Kristo mwanane na kuja kufa kwa ajili yetu na kuondoa sheria ya dhambi na mauti iliyoletwa na shetani, na kuweka sheria ya uzima ndani ya kila atakaye muamini. Ukiamua kumwamini Kristo Yesu, basi hakutakuwa na hukumu ya dhambi na mauti juu yako kwasababu sheria ya roho wa uzima inakuweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. Na hii inawezekana kwasababu wewe utakuwa hauenendi tena katika mwili ambao ni dhaifu kupokea sheria za Mungu, bali uko katika roho ambamo sheria ya Mungu inawekwa ndani yako automatically, wala hutakuwa na haja ya kutumia nguvu kuacha dhambi. Utajikuta tu unajua hii ni dhambi na hivyo utaachana nayo au utakaa mbali nayo.

Mpendwa msomaji ukiona bado unatumia nguvu sana kuacha dhambi na kwa muda mrefu, nakusihi ujichunguze kwa habari ya wokovu wako kwasababu hutakiwi kuishi na tamaa za mwili wakati unatakiwa kutawaliwa na Roho Mtakatifu ili akuweke huru mbali na dhambi na mauti.

Thursday, 4 May 2017

Namna ya kumlilia Mungu katika shida yako



Zaburi 107:19-20 inasema “Wakamlilia Bwana katika shida zao. Akawaponya na shida zao.Hulituma neno lake huwaponya. Huwatoa katika maangamizi”

Ashukuriwe Mungu aliye juu kwakuwa tunalo tumaini katika yeye. Kwakuwa ndiye ngome yetu na msaada wetu wakati wa mateso.

Leo ningependa nikukumbushe kwa habari ya kumlilia Mungu katika shida uliyonayo.Kwa maana imeandikwa muite Mungu maadamu anapatikana.

Mara nyingi tunakuwa katika shida na taabu katika maisha yetu na tunakaa hapo hapo katika hiyo shida kwa muda mrefu sana kuliko ilivyotakiwa. Ni kwanini? Hii ni kwasababu hatumlilii Mungu katika shida zetu. Unaweza kujiuliza mbona huwa ninaomba sana lakini majibu hayaji. Hii pia ni kwasababu unaomba vibaya. Imeandikwa kuwa” hampati kwasababu mnaomba vibaya”.

Kuomba vibaya ni kwa namna gani?
Ni kwa kulalamika na kuliangalia tatizo lako zaidi ya kumuangalia Mungu na uweza wake wa kuliondoa tatizo. Mara nyingi unakuwa na maombi yanayotokana katika nafsi yako kuliko yanayotoka rohoni. Rohoni ni mahali pasipo na waa na ndipo Mungu hukaa. Kwenye nafsi yako ni mahali unafanya maamuzi kutokana na hali halisi inayokuzunguka. Hivyo kuomba vizuri ni kuomba sawasawa na neno la Mungu, na si mapenzi yako.
Tukiweza kuomba sawasawa na neno lake, atasikia. Mara kwa mara tunaomba sawasawa na mapenzi yetu, na ndipo Mungu hatusikiii kwasabau hujaingia bado kwenye himaya yake. Kulia sana na uchungu sana hausaidii na tena imeandikwa “uchungu wote na uondoke kwenu.”

Embu chunguza hayo unayomuomba Mungu na namna unavyomuomba, je unaomba kwa hisia ya mwilini au katika roho? Mungu ni roho, ukitaka kuongea nae uwe katika roho na ndipo Roho Mtakatifu hutusaidia pale tunaposhindwa kuomba katika roho.

Nakusihi uanze kutafuta kujua namna ya kumuomba Mungu katika roho na utaona jinsi majibu utakavyoyapata kwa haraka kama neno linavyosema walimlilia, wakaponywa na kuondolewa katika maangamizi yao.

Mungu yuko tayari kukupa hitaji lako unalomuomba, ni wewe ambaye unachelewa kujua mapenzi yake ili uweze kupata haja za moyo wako.