Sunday, 4 February 2018

Maisha Ya Amani

Karibu msomaji wangu

Leo tunajifunza kuhusu AMANI.

Nini maana ya Amani. Amani ni ile hali ya kuishi bila wasiwasi au mashaka ya aina yoyote.
Amani ni hatua ya juu sana ya maisha ya mtu yenye kutamaniwa. Palipo na amani ndipo mtu anapenda kuishi hapo.

Ni namna gani mtu anaweza kuishi maisha ya Amani?
Ngoja tuone fomula ifuatayo ili kuweza kupata amani.

IMANI - HOFU = AMANI

Ndiyo, ukiwa na imani katika kitu fulani, halafu ukatoa hofu inayokuzunguka basi utakuwa na amani. Ukiifahamu hii fomula na kuifanyia kazi, itakusaidia kuvuka salama katika maeneo mengi unayoyapitia katika maisha yako.

Ukisoma Waebrania 11:1 inasema "Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana."
Ukiwa unaamini neno la Mungu kuhusu jambo fulani katika maisha yako, na ukiondoa hofu inayokuzungukia juu ya hilo jambo, utakuwa na Amani.

Hofu ni kule kuangalia hali inayokuzunguka na kukuogopesha. Inaweza kuwa ya wakati huohuo au ya kufikirika kwa wakati ujao.

Ili kuweza kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, usiwe mtu wa hofu. Ondoa hofu katika kila unalolifanya. Wewe amini tu kuwa unaweza au inawezekana kupona ugonjwa huo, kupata kazi nzuri, kupata ndoa nzuri, kupata watoto wema, kuwa mtu muhimu n.k. Hii ndiyo imani.

Usiangalie ni hali gani unayoipitia kwa sasa, bali macho yako yaone kile unachokiamini na ndipo utapata Amani na pole pole utaanza kuona kile kitu unachoamini kinatokea.

Mara zote hofu ndiyo inayokufanya usipige hatua, na unakuwa sikuzote mtu wa sintofahamu. Yaani sijui itakuwaje katika kila jambo. Ukiona hali hiyo ujue uko katika hofu.

Amua leo kuondoa hofu katika maisha yako na uamini kile alichosema Mungu kuwa utaweza na utapata. Hapo utaanza kuona maisha yako yanabadilika na kuwa ya Amani.