Karibu kwenye somo la leo.
1 Yohana 3: 1 inasema “Tazameni ni pendo la namna gani
alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwasababu hii
ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.”
Ni jambo la kushukuru sana kuitwa mtoto wa mtu mkubwa,
maarufu na mwenye utajiri mwingi hapa duniani.
Na hii ni kwasababu unajua ya kuwa matatizo utakayoyapata yatatatuliwa kwa haraka na bila
shaka kabisa. Mtu mwenye uwezo wa kifedha na
maarifa ni mtu anayeweza kutatua changamoto zake kwa uraisi zaidi kuliko
mtu asiye na fedha na maarifa. Ndiyo maana watoto wa matajiri wanakuwa na hali
nzuri zaidi kimaisha kuliko watoto wa masikini.
Tukiangalia neno letu la leo tunaona ya kuwa tumeitwa wana
wa Mungu na ndivyo tulivyo kama ilivyoandikwa pia kwenye Yohana 1: 12 inayosema “ Bali wote
waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu, ndio wale waliaminio jina
lake;” Wewe kama umempokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, ujue
tayari wewe ni mtoto wa Mungu.
Naomba tumuangalie huyu
Mungu wetu alivyo ili tuweze kujua ni kwa namna gani wewe kama mtoto wake
unatakiwa kuishi hapa duniani.
Mungu wetu ni mwenye uweza wote, ndiye aliyeziumba mbingu na
dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Ndiye mwenye kusamehe
dhambi, Mungu ndiye mwenye dhahabu zote na fedha zote. Mungu anawalinzi ambao
ni malaika wanaotulinda na kutuletea haja zetu usiku na mchana. Mungu ndiye
mwenye kutupa pumzi ya uhai ili tuishi. Mungu hashindwi na lolote. Mungu ndiye
mwenye mipango yako yote na ndiye mwenye kujua kila kitu katika maisha yako.
Ukiomba chochote kwa Mungu sawasawa na mapenzi yake anakupa.
Mpendwa msomaji wangu, hivi kama huyu ndiye Mungu ambaye ni
baba yako na wewe ni mtoto wake, umesha
wahi kujiuliza mbona maisha yako hayafanani na uweza wake? Huenda tatizo ni sisi wenyewe kwa kutokumjua
vizuri Mungu wetu na anataka nini kwetu.
Mara nyingi sisi tulioitwa watoto wa Mungu tunaishi maisha
ambayo yanamichanganyo. Kwa Mungu kidogo, na kwa dunia kidogo. Tumeona katika
hili neno ya kuwa dunia haiwatambui wana
wa Mungu, kwasababu hawakumtambua Mungu. Hii ina maana gani? Ukiwa kama mwana
wa Mungu ni lazima utakuwa tofauti na dunia, kwa kuvaa, muonekano, kuongea na
hata namna unavyoishi. Na kwasababu ya tofauti hizo, dunia inashindwa kukuelewa
kwasababu vile vitu ambavyo wao wanavikimbilia, wewe huvikimbilii. Kama wewe ni
makini wa kufuatilia maneno ya Mungu, utagundua vitu vingi ambavyo vinaendelea
duniani ni kutoka kwa yule mwovu.
Tuangalie mfano mmoja wa mavazi, watu wa Mungu ambao ni
kanisa lake kuna namna ambayo wanatakiwa kuonekana kama vile wanawake wasivae nguo
fupi au wasivae suruale, na pia wasijipambe kwa dhahabu na kusuka nywele za bandia na
mapambo ya usoni (cosmetics). Haya yote
yanaitwa ni machukizo mbele ya Mungu ambaye ni baba yetu. Kama wewe bado
unafanya mambo kama hayo, ujue unamchukiza baba yako na unafanya mambo ambayo
ni ya kidunia na kuacha mpango mzima wa Mungu katika maisha yako.
Mungu wetu anataka tuwe safi bila mawaa katika maisha yetu
na siyo michanganyo ambayo mwishowe atakutapika siku zijazo.
Je wewe ni mwana wa Mungu nabado uko katika michanganyo hii
ya dunia? Huenda ndiyo maana mambo yako hayaendi na kila ukiomba unaona kama
unagonga mwamba. Ondoa unajisi katika maisha yako na uone jinsi Mungu ambaye ni
baba yako wa mbinguni atakavyoshuka na kukuhudumia. Usimpe shetani nafasi kwa
chochote katika maisha yako.
Soma zaidi maandiko yafuatayo kuhusu namna Mungu anavyopenda
uwe na utagundua kumbe ni kinyume kabisa na namna dunia inavyotaka uwe.
1Wakorintho 14:34-35, 1Wakorintho 11:1-15, 1Timothy 2: 8-15,
1 Petro 3:3-5